Vyama vya upinzani vinavyojikongoja kufanya kampeni Zanzibar

Unguja. Tangu Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ifungue pazia la wagombea wa vyama vya siasa kufanya kampeni za kuomba kura kwa wananchi Septemba 11, 2025, baadhi ya vyama vya siasa bado vinajikongoja kufanya hivyo Zanzibar.

Wagombea urais wa vyama 11, kati ya 17 waliochukua fomu, ndiyo waliteuliwa na ZEC kupeperusha kuwania nafasi hiyo.

Wagombea wengine wa vyama vitano walishindwa kurejesha fomu na mmoja wa Chama cha Wananchi (CUF), licha ya kurejesha fomu, alishindwa kukidhi kigezo cha kupata wadhamini kwa mkoa mmoja kati ya mitano.

Hata hivyo, zikiwa zimepita wiki mbili sasa tangu kampeni zianze, ukiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo, baadhi ya vyama bado havijazindua kampeni zake huku vingine vikiishia kufanya mkutano mmoja tu wa uzinduzi.

Vyama ambavyo havijazindua kampeni hadi sasa ni NCCR Mageuzi ambacho kimesema kwamba kinatarajia kufanya hivyo Septemba 28, mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi, mgombea urais kupiti chama hicho, Laila Rajab Khamis amesema wanatarajia kuzindua kampeni zao Septemba 28, 2025 katika kiwanja cha Kibandamaiti Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema wamechelewa kuzindua kampeni hizo kwa sababu walikuwa wanasubiri viongozi wa kitaifa.

“Tulikuwa tunasubiri viongozi wetu, walizindua Dar es Salaam, sasa wanakuja huku ndio walitupangia hivyo,” amesema.

Vyama vingine ambavyo vimefanya mkutano mmoja tu wa uzinduzi ni UPDP ambacho kilizindua kampeni Septemba 14 katika viwanja vya Garagara, Mtoni Kidatu, Mkoa wa Mjini Magharibi, NLD na TLP.

Mgombea urais wa TLP kupitia chama hicho, Hussein Juma Salum amesema wanatarajia kufanya mkutano mwingine kati ya Septemba 30 au Oktoba mosi kumnadi mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Hata hivyo, amesema bado ni matazamio, huenda kukawa na mabadiliko. Kuhusu kukaa muda mrefu bila kufanya kampeni za uchaguzi, amedai kwamba huo ndio mpango wa chama.

Wakati akieleza hayo, mgombea urais wa NLD, Mfaume Khamis Hassan amesema wanatarajia kufanya mkutano wa pili Septemba 24.

Vyama vingine ambavyo vimezindua kampeni na kufanya mikutano miwili ni Ada-Tadea, ADC, AAFP na Makini.

Hata hivyo, baadhi ya wagombea wa vyama hivyo walipoulizwa kuhusu kampeni zao kujikongoja, wamesema “wanazifanya kisayansi ili kuendana na hali halisi ya mazingira.”

“Hii ni mipango, kampeni unaangalia sera na namna ya kuwafikia wananchi lakini sio lazima kukaa kwenye majukwaa, badala yake unaweza kupita kwa watu ukaomba kura,” amesema Ameir Hassan Ameir mgombea urais kupitia chama Makini

Ameir amefanya kampeni zake kwa staili ambayo pia imetumiwa na wagombea wa CCM na ACT -Wazalendo kwa kutembelea makundi na kuzungumza nayo, hivyo na yeye ametembelea masoko ya Mwanakwerekwe kusaka kura za wafanyabiashara.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza hali hiyo katika sura mbili tofauti; moja, ni ukata unaovikumba vyama hivyo na nyingine ni kutokana na baadhi ya vyama kutokuwa na ushawishi kwa wananchi.

Abdi Juma Issa, mchambuzi wa siasa amesema kuna mambo kadhaa yanayofanya vyama vishindwe kuendesha kampeni za kila siku.

“Ukiangalia mfumo mzima wa vyama hivi utagundua kwamba havina rasilimali kubwa, si tu za kifedha, bali hata wafuasi walionao ni wachache, kwa hiyo inakuwa kazi ngumu kuzunguka kila siku ilhali anajua anachokwenda kupata ni kidogo,” amesema.

Mchambuzi mwingine, Salim Mfaume amesema si mara ya kwanza kwa baadhi ya vyama vya siasa kusuasua kufanya kampeni, kila uchaguzi huwa vinakutana na changamoto hiyo kutokana na uhaba wa rasilimali fedha.

Akizungumza kuhusu kupewa magari na kujaziwa mafuta, Mfaume amesema hilo halitoshi kwa sababu kampeni sio tu usafiri wa mgombea, badala yake zinahusisha vitu vingi kwa ajili ya kuandaa mazingira wezeshi katika eneo zinapofanyika kampeni hizo.

Licha ya hali hiyo, katika kampeni za baadhi ya vyama hivyo, wagombea walitoa ahadi mbalimbali iwapo wakiingia madarakani, zaidi zikijikita katika kutatua changamoto ya ajira, ujenzi wa viwanda, kuimarisha zao la karafuu na kutoa mishahara minono kwa wafanyakazi wa Serikali.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia UPDP, Hamad Mohamed Ibrahim amesema iwapo akipata ridhaa ya kuingia madarakani, Serikali yake itajikita katika kujenga viwanda kwa ajili ya kuchaka karafuu.

Pia, amesema vijana wataoa bure na mahari zitatolewa na Serikali huku mwanamke anayechumbiwa atapewa Sh1.5 milioni kwa ajili ya kujikimu kimaisha.

“Serikali ya UPDP itajikita kwenye viwanda, tutajega viwanda vya kuchakata karafuu, tunataka karafuu itakayokuwa inauzwa nje asilimia 80 iwe imeshachakatwa ndani, amesema.

Katika kuliendea vema jambo hilo, UPDP inategemea kujenga vinu vya nyukilia ili kukabiliana na changamoto ya umeme ambao utaendesha viwanda na matumizi ya nyumbani

“Lile suala la kukatika umeme, vitu vinaharibika linakwenda kuwa mwisho, tunaomba mtuunge mkono ili kuleta mabadiliko katika nchi yetu,” amesema.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wakulima AAFP, Said Soud Said amesema iwapo akipata ridhaa ya kuingia ikulu, kilo moja ya karafuu itauzwa Sh50, 000 ili wakulima wanufaike na kilimo chao.

Pia, amesema Bandari ya Zanzibar itakuwa ni bure kuingiza mizigo kwani tozo zinazotozwa katika bandari ni kubwa kuliko gharama ya mzigo.

Alieleza hayo katika mkutano wake Septemba 18, 2025 katika uwanja wa Mabembea Malindi Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Inasikitisha leo hii mkulima wa karafuu hana hata baiskeli lakini anayekwenda kununua karafuu anaendesha gari aina ya Prado, huu ni unyonyaji,” amesema.

“Naomba mnipeleke ikulu ili tupate ufumbuzi huu wa changamoto zinazotukumba,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea urais wa TLP, Hussain Juma Salum amesema akichaguliwa kuiongoza Zanzibar atahakikisha anawarahisishia wananchi na kuwa na maisha bora pamoja na kuendeleza amani iliyopo na demokrasia.

Akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni wa chama chake Septemba 20, alisema TLP itaimarisha uchumi kwa kutafuta fursa mpya zilizopo kutokana na kukuwa kwa teknolojia.

Aidha mgombea huyo wa urais amewahimiza vijana kufanya kazi kwani wao ndio tegemeo la taifa.

Pia chama hicho kimesema wakikichagua kitahakikisha wakulima wanapatiwa pembejeo ili walime kilimo chenye tija na kuendelea kuwa tegemezi kwa Taifa.

Mgombea wa urais Zanzibar wa Afrika Democratic Allience (Ada-Tadea), Juma Ali Khatib amesema pamoja na kuingia kwenye ushindani huo akitarajia nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais, anasema iwapo ikitokea akachaguliwa watawekeza nguvu zaidi katika elimu ya amali.

“Sababu ya chama hicho kufanya hivyo ni kuona kuwa elimu ya ufundi na amali inapewa kipaumbele kikubwa kwa vizazi wananchi wake,” amesema Juma.

Mbali na hilo, amesema chama hicho kitajikita katika masuala ya uvuvi kwa kuwa na meli kubwa za uvuvi.

Mgombea urais kwa tiketi ya NRA, Khamis Faki Mgau amesema iwapo atapata ridha ya kuchaguliwa na wananchi ya kuongoza Zanzibar, atahakikisha anaboresha masilahi ya wafanyakazi wakiwemo ya walimu kwa kima cha chini cha mshahara wa Sh1.5 milioni kwa ngazi ya cheti.

Amesema bado masilahi ya walimu ni madogo kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kufundisha vijana, hivyo atakapopata ridha atayaangalia kwa karibu masilahi ya walimu.

Amesema kazi ya ualimu ni ngumu hivyo inahitaji kutuliza akili bila kuwa na mawazo ya aiana yoyote.

“Mtakaponichagua kuiongoza nchi, nitayaangalia masilahi ya walimu kwa kuwaongezea mshahara milioni moja na nusu kwa ngazi ya cheti,” amesema Mgau

Mgombea urais wa Alliance for Demoratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohammed amesema iwapo wananchi watampa ridhaa kumchagua kuwa Rais wa Zanzibar, ndani ya siku 100 za kwanza, atahakikisha bei ya mchele wa mapembe haizidi Sh1,500.

Amesema suala hilo linawezekana kwa kupunguza kodi au kuondosha kabisa, jambo ambalo litampunguzia mwananchi gharama za maisha.

Aidha amesema pia atatoa vifaa vya kilimo ikiwemo pembejeo bure kwa wakulima ili waweze kuzalisha mchele wa kutosha na kuacha kutengemea Mchele kutoka nje ya Zanzibar.

“Mtakaponichagua kuwa Rais wa Zanzibar, nitapunguza bei ya mchele, kilo moja ya mapembe haitazidi Sh1, 500 ili kuwapa unafuu wananchi kumudu gharama za maisha,” amesema.