Iringa. Madaktari bingwa 45 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamewasili mkoani Iringa ambako watatoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa wananchi takribani 3,000, ambao wamekuwa wakilazimika kusafiri nje ya mkoa kufuata huduma hizo.
Akizingumza leo Septemba 23, 2025 wakati wa kuwapokea madaktari hao watakaoweka kambi mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amesema uwepo wao utasaidia kupunguza gharama za wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma kwenye hospitali za kanda na mikoa mingine.
“Nawasihi wananchi kuichukulia kwa uzito fursa hii adimu, hivyo tujitokeze kwa wingi tuweze kufahamu afya zetu kwa kupata uchunguzi wa kibingwa,” amesema.
Amesema huduma hizo zinatarajiwa kuwajengea uwezo madaktari mkoani Iringa, kwani wataweza kubadilishana ujuzi na uzoefu katika taaluma.
Mratibu wa kambi hiyo ya madakatari kutoka Wizara ya Afya, Dk Ulimbakisye Macdonald amesema madaktari hao bingwa wamejipanga kutoa huduma kwa ufanisi kwa wagonjwa watakaojitokeza.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Sylivia Mamkwe, amesema ni ujio wa awamu ya nne ya madaktari bingwa mkoani humo.
Amesema katika awamu ya tatu zaidi ya wananchi 2,000 walipatiwa huduma.
Dk Mamkwe amesema miongoni mwa huduma zitakazotolewa ni za magonjwa ya wanawake, ya ndani, kinywa na meno, pamoja na upasuaji.
Kambi hiyo imeanza Septemba 22, 2025 na inatarajiwa kufikia tamati Septemba 26, katika hospitali za wilaya zilizopo katika halmashauri tano za Mkoa wa Iringa.