Dar es Salaam. Mshtakiwa Jasmine Elphas na wenzake 10, wanaokabiliwa na mashtaka 20 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7bilioni kwa udanganyifu mali ya Benki ya Equity Tanzania Limited, wataendelea kusalia rumande hadi Oktoba 6, 2025 wakati kesi hiyo itakapotajwa.
Hatua hiyo, inatokana na upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi kutokamilika, huku mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na uhujumu uchumi namba 18447 ya mwaka 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbali na Elphas ambaye alikuwa ni ofisa wa benki ya Equity makao makuu, pia yupo mfanyabiashara Fredrick Elphas Ogenga.
Wengine ni Caroline Masayanyika na Lilian Koka, ambao pia walikuwa maofisa wa benki hiyo kutoka makao makuu ya benki hiyo.
Pia, yupo Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul, Claude Beda na Jefferson Ogenga, wote wakiwa ni wafanyabiashara.

Leo Jumanne, Septemba 23, 2025 wakili wa Serikali Tumaini Mafuru ameieleza Mahakama hiyo, kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo wanaomba mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Mafuru ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo wakati kesi hiyi ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Kutokana na upelelezi kutokukamilika hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 6, 2025 itakapotajwa.
Hata hivyo, kesi hiyo imeahirishwa kwa njia ya video huku washtakiwa wakiwa rumande.
Hata hivyo, mshtakiwa Caroline amefutiwa mashtaka ya utakatishaji fedha yanayomkabili.
Kwa mujibu wa mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Agosti 30, 2024 hadi Juni 28, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya jijini Dar es Salaam, waliongoza genge la uharifu na kujipatia Sh5.7bilioni mali ya Benki ya Equity Tanzania Limited.
Katika tarehe hizo mshitakiwa Jasmine na Ogenga, wakiwa ndani ya Makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, waliiba Sh3.6 bilioni zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika Akaunti ya Clearing and Settlement mali ya Benki ya Equity.
Mshtakiwa Caroline katika tarehe hizo, akiwa katika Makao Makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, anadaiwa kuiba Sh728 milioni mali ya benki hiyo.
Pia, ilidaiwa, kati ya Februari 28 na Aprili 2, 2025 makao makuu ya benki hiyo, Lilian aliiba Sh26 milioni kutoka akaunti ya benki hiyo.
Vilevile, kati ya Januari Mosi hadi Aprili 24, 2025 katika benki hiyo, Maina aliiba Sh101 milioni mali ya benki hiyo.
Ilidaiwa, kati ya Januari 22 hadi Aprili 24, 2025 katika ofisi hizo za benki hiyo Mohamed, aliiba Sh57 milioni, huku Fata akidaiwa kuiba Sh758 milioni, tukio analodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2, 2024 hadi Mei 25, 2025.
Mahakama ilieleza kuwa, kati ya Januari 9, hadi Mei 25, 2025, Makao Makuu ya Benki ya Equity iliyopo Ilala, Mrisho aliiba Sh211 milioni, mali ya benki hiyo.
Upande wa mashtaka ulidai, kati ya Januari 9 hadi Mei 28, 2025 makao makuu ya benki hiyo, mshtakiwa Neema aliiba Sh32 milioni mali ya benki hiyo.
Vile vile siku na eneo hilo, Beda anadaiwa kuiba Sh108 milioni, mali ya benki hiyo.
Pia, ilidaiwa, washitakiwa wote isipokuwa Caroline, wanakabiliwa na mashitaka 10 ya utakatishaji wa fedha walizodaiwa kuiba.