Wawili wafariki dunia Kilimanjaro katika matukio mawili tofauti

Moshi. Mkazi wa Kijiji cha Kimbogho Kata ya Mamba Kusini Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Claudia Temba (68) amefariki dunia baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kuteketea kwa moto ambao chanzo chake hakijafahamika.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Jumanne Septemba 23, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema tukio hilo limetokea leo na tayari uchunguzi wa awali umeanza ili kubaini chanzo cha moto huo.

“Ni kweli limetokea tukio la ajali ya moto ambapo mtu mmoja  alifariki dunia baada ya mwili wake kuteketea ndani ya nyumba anayoishi ya vyumba viwili,” amesema Kamanda Maigwa. 
Amesema moto huo umeteketeza mali zilizokuwemo ndani.

“Chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa, mabaki ya mwili wa marehemu yamefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa taratibu za mazishi,” amesema Kamanda Maigwa 
Katika tukio jingine, mwanaume mmoja mwenye umri kati ya miaka 40-45 ambaye jina lake halijafahamika, amekutwa amefariki dunia  kando mwa barabara kuu ya Mwanga -Moshi.


“Septemba 21 huko maeneo ya Kijiji cha Kichwa cha Ng’ombe Wilaya ya Mwanga, ulipatikana mwili wa mtu asiyefahamika jina akiwa amefariki dunia kwenye eneo la pori la Mfolo umbali wa mita 70 kutoka barabara kuu ya Mwanga -Moshi,” amesema Kamanda Maigwa. 

Aidha, Kamanda Maigwa amesema chanzo cha kifo hicho bado kinachunguzwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya cha Kisangara kusubiri uchunguzi zaidi wa kidaktari na utambuzi.