STAA mpya wa Yanga, Celestine Ecua amesema amesikia kila kitu kuhusu mashabiki wanaomsema kwamba yeye ni mchoyo wa kutoa pasi kwa wenzake uwanjani, kisha akatoa msimamo kuwa, haoni tatizo kwake kuanzishwa benchi kwa sababu anajua uwezo alionao.
Ecua aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast aliyokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka Zoman pia ya huko akiwa na rekodi ya kufunga mabao sita ndani ya nusu msimu, alisema kama mchezaji kuna wakati anaamua kujitoa kwa nia ya kuisaidia timu na si kuwa mbinafsi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ecua alisema kazi kubwa ya kila mchezaji ni kuisaidia timu kufanya vyema na sio kuwania nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza, hilo ni suala la kocha kutokana na mahitaji ya mechi husika.
“Mimi si mchoyo uwanjani kama ambavyo watu wanasema na ninajua kucheza kwa ushirikiano, jambo ambalo mashabiki wataliona katika mechi zijazo. Michuano ndio kwanza imeanza ni mapema sasa kusema mambo mengi ila kinachohitajika ni kukamilisha malengo ya timu na kuhakikisha unapata nafasi ya kucheza bila kuchambua sana,” alisema Ecua na kugusia ishu ya kuanzia benchini.
“Hatua ya kuanzia benchini ndani ya timu hiyo wala sio kitu kinachonisumbua, kwani naendelea kujipanga kujipa muda zaidi wa kucheza kupitia muda ninaopatiwa sasa. Ndani ya kikosi kila mchezaji ana kipaji kikubwa ndio maana wale wanaoanza na hata wanaoingia wamekuwa wanahusika kutengeneza ushindi,” alisema Ecua na kuongeza;
“Kwa wala sioni shida kuanzia benchini na hiyo haimaanishi anayeanzia benchini, sio mchezaji bora ila ni fikra tu za watu.”
Ecua ametua Jangwani huku nafasi anayocheza ikiwa ina mastaa kama, Pacome Zouazoua, Maxi Nzegeli na Mohamed Doumbia ambao wote wanakwenda kuongeza uimara mkubwa kwenye eneo hilo.
Pia kuna Clement Mzize, Andy Boyeli na Prince Dube pale anapotaka kutumika kama mshambuliaji wa kati, nafasi anayoimudu pia.Katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa alitokea benchini, huku ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba alianza katika kikosi cha kwanza.