Mtwara. Baada ya kufanya kampeni katika mikoa 13, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuingia katika Mkoa wa Mtwara kunadi sera za chama hicho akiomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Tanzania.
Tangu chama hicho kizindue kampeni zake za uchaguzi Agosti 28, 2025 jijini Dar es Salaam, mgombea huyo amepita mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Dodoma, Songwe, Njombe, Mbeya, Iringa, Singida, Tabora na Kigoma.
Mikoa mingine ni Kusini Pemba, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Ruvuma, kote huko amenadi ilani ya CCM 2025/2030 kabla ya leo kuingia Mtwara ambapo anatarajiwa kuwepo kwa siku mbili akifanya mikutano minne katika wilaya za Masasi na Mtwara.
Mkoa wa Mtwara ambao unajulikana kwa utajiri wa gesi asilia, mazao ya korosho pamoja na fursa za bandari ya kimkakati, umekuwa ukitazamwa kama kitovu cha maendeleo katika Kanda ya Kusini.
Wananchi wengi wamekuwa na shauku kubwa ya kumsikiliza mgombea huyo, wakitarajia atagusia changamoto zao na kutoa dira ya mustakabali wa maendeleo ya mkoa.
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliozungumza na Mwananchi wameeleza matarajio ya kile wanachotaka kusikia kutoka kwa mgombea huyo akionesha namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo.
Mkoa huo unaojulikana kama kinara wa uzalishaji wa zao la korosho nchini, wakulima wake wamekuwa wakilalamikia bei ya zao hilo kutokuwa ya uhakika, changamoto za pembejeo, pamoja na ucheleweshaji wa malipo.
Matarajio ya wananchi ni kusikia ahadi za kisera zitakazohakikisha bei ya korosho inakuwa yenye tija, sambamba na kuongeza thamani kwa kusimamia viwanda vya kubangua na kusindika zao hilo ndani ya mkoa.
“Tunataka kuona korosho zetu zinapata thamani zaidi. Tunategemea kiongozi atakayehakikisha mkulima anafaidika moja kwa moja na jasho lake,” amesema Fatuma Mbarouk, mkulima na mkazi wa Mangaka.
Kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini, vijana wa Mtwara wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira licha ya mkoa wao kuwa na rasilimali nyingi, hivyo matarajio yao ni kusikia sera za kuhakikisha miradi ya maendeleo inawapa nafasi za ajira za moja kwa moja.
“Mtwara tuna gesi, tuna bandari, tuna mazao ya biashara, lakini bado vijana wengi hawana kazi. Tunataka kuona mipango ya ajira ya uhakika,” anasema Saidi Omari, mkazi wa Nanyumbu.
Aidha, wananchi wa vijijini wameeleza kiu yao ya kupata huduma bora za afya na maji safi. “Wakati mwingine tunatembea zaidi ya kilometa tano kutafuta maji. Tunatarajia Serikali iweke kipaumbele kwenye miradi ya maji vijijini,” anasema Asha Ali, mkazi wa Mangaka.
Kwa upande wake, Sheikh Suleiman Mohamed ambaye ni kiongozi wa dini, amesema matarajio ya viongozi wa dini mkoani humo ni kuona nchi inaendelea kuwa na mshikamano na amani.
“Tunataka kampeni hizi ziwe za kistaarabu. Muhimu zaidi ni kuona Serikali itakayoingia madarakani inaleta mshikamano na maendeleo, siyo migawanyiko,” amesema Sheikh Mohamed.