Zitto aahidi kuanza na barabara, Kata ya Businde

Kigoma. Mgombea ubunge wa Kigoma Mjini, kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema akishinda ubunge na wananchi wakampa madiwani wa chama hicho wataifungua Kata ya Businde kwa kuboresha miundombinu ya barabara.

Akizungumza leo Jumanne, Septemba 23,2025 katika mkutano wa kampeni uliyofanyika Kata ya Businde, Zitto amesema kutokana na ubovu wa barabara ya kata hiyo wananchi hutumia gharama kubwa za  usafiri kuanzia Sh4,000 kwenda mjini kufanya shughuli zao kwa bodaboda.

Amesema wakichukua halmashauri jambo la kwanza ni kuhakikisha wanawekeza miundombinu ya barabara katika kata pamoja na kurudisha mradi wa barabara ya Kasulu kupitia Msimba –Ujiji, ambao kwa kipindi chake aliuanzisha na kuomba fedha kutoka Benki ya Dunia.

“Wakati nikiwa mbunge kwa kipindi changu mwaka 2015-2020 tuliweza kuomba mradi kutoka Benki ya Dunia na tulifikia eneo nzuri, lakini baada ya muda wangu kuisha mradi huo ulikufa kwa sababu hakuna aliyefuatilia tena,” amesema Zitto.

Naye mgombea udiwani kata ya Businde, Said Makala amesema kuna maneno mengi yanaendelea, lakini wasidanganyike kwani wananchi hao wanajua uwezo wake wa utendaji kazi.

“Changamoto zipo nyingi katika kata yetu na mkinichagua nitaweza kuzifanyia kazi moja baada ya nyingine, hivyo naomba kura zenu niweze kuwatumikia wananchi wa Businde,” amesema Makala.

Katibu wa chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Yunus Luhovya amesema chama hicho kilipokuwa kinaongoza halmashauri hiyo kiliweza kufanya maendeleo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara za kiwango cha lami.

“Unapompoteza mbunge kama Zitto unakuwa umepoteza masilahi ya wananchi, hivyo niwashauri wananchi tarehe 29, msifanye makosa katika hilo,”amesema Luhovya.