Iringa. Watuhumiwa 10 wakazi wa Donbosco, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa kwa mara ya kwanza leo wakishtakiwa kwa mauaji ya kukusudia yenye namba PI 23302/2025.
Inadaiwa kuwa Septemba 11, mwaka huu, watuhumiwa hao walimshambulia na kumsababishia kifo mtoto Yohana Mgaya mwenye umri wa miaka 14 katika mtaa wa Donbosco kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa.
Akisoma hati ya mashtaka leo Septemba 24, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Rehema Mayagilo, Wakili wa Serikali, Saul Makori ameeleza kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na kosa la mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.
Watuhumiwa wakazi wa Donbosco, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa wakiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa kwa mara ya kwanza leo wakishtakiwa kwa mauaji ya kukusudia yenye namba PI 23302/2025 Donbosco kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa.
Watuhumiwa waliotajwa mahakamani ni Gloria Kyando, Farida Kamwagira, Rahabu Nsilu, Mussa Chondoma, Vasco Sanga maarufu kama Mkenya, Teodosia Msilu, Bosco Kabogo, Zawadi Msele, Evelina Chadewa na Erasto Kilamlilo.
Hata hivyo, watuhumiwa hao hawakuruhusiwa kujibu kitu kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji, hivyo washtakiwa walirudishwa mahabusu hadi Oktoba 8, 2025 kesi hiyo itakapotajwa tena.
Aidha awali Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa lilitoa ufafanuzi kuhusu tukio la kusikitisha lililoonekana kwenye mitandao ya kijamii likimuonesha Yohana Mgaya (14), akipigwa na kundi la watu waliomtuhumu kwa wizi huku Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa, Allan Bukumbi akieleza kuwa kijana Mgaya alituhumiwa kuhusika na matukio ya wizi wa mali mbalimbali ikiwemo vifaa vya bajaji, simu, nguo na parachichi, kabla ya kushambuliwa hadi kufariki dunia mnamo Septemba 11, 2025.
Watuhumiwa wakazi wa Donbosco, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa wakiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa kwa mara ya kwanza leo wakishtakiwa kwa mauaji ya kukusudia yenye namba PI 23302/2025 Donbosco kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa.
Pia Kamanda Bukumbi alieleza kuwa marehemu Mgaya alikuwa ameachiwa kutoka gerezani Julai 2025 kwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha.