Askofu Munga azikwa, jamii ikiaswa juu ya upendo

Mkinga. Mazishi ya Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Stephen Munga, yametawaliwa na nasaha za kuwaasa Watanzania kuimarisha amani na upendo, badala ya kujenga chuki.

Dk Munga amezikwa leo, Septemba 24, 2025, saa 9:30 alasiri ndani ya kanisa lililopo Kijiji cha Maramba, wilayani Mkinga, mkoani Tanga.

Mkuu wa KKKT Tanzania, Askofu Alex Malasusa, amesema kifo cha Askofu Munga kimeacha funzo kuwa katika maisha hakuna nafasi ya chuki, bali ni upendo.

Amesema, pamoja na misukosuko aliyopitia Askofu mstaafu Munga wakati wa utumishi na baada ya kustaafu, bado alionesha unyenyekevu wakati wote na kukubali kukutana na upande mwingine ili yafanyike mazungumzo ya kumaliza tofauti.

“Niwaambie kuwa, tulishakuwa katika mazungumzo ya kumaliza tofauti zilizokuwapo na mazungumzo yalishafikia hatua nzuri mno,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kilama, amesema alikutana na Askofu mstaafu Munga siku chache kabla ya kifo chake, katika mazungumzo yao alisisitiza mambo matatu ambayo ni utii, uvumilivu na kusameheana.

“Tumuenzi Askofu Munga kwa kusimamia mambo makuu matatu aliyoyaishi, ambayo ni utii, uvumilivu na kusameheana,” amesema alipotoa salamu za Serikali wilayani Mkinga.

Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga, Dk Phillip Baji, amesema katika kipindi cha uongozi wake wa kiroho, Askofu Munga alikuwa kiongozi aliyekubali kukosolewa na hakusita kukosoa pale alipoona mambo hayaendi sawa.

“Kutokana na msimamo wake, kuna wakati alijikuta akiwa katika hali ngumu, kwa kuwa wengine hawataki kukosolewa,” amesema.

Amesema alikuwa mbunifu ambaye, kwa kushirikiana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini chini ya ulezi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa, aliasisi mchakato wa kuanzisha chuo kikuu.

Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk Maimbo Mndolwa, ni miongoni mwa walioshiriki ibada ya mazishi iliyohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa dini wa madhehebu mengine.

Mwili wa Dk Munga ulitolewa nyumbani saa 4:20 asubuhi kwa maandamano na kupelekwa kwenye Kanisa la Anglikana lililo jirani na makazi yake, ambako umezikwa. Kanisa hilo imeelezwa kuwa Dk Munga alipokuwa Maramba ndiko alikokuwa akiabudu.

Dk Munga alifariki dunia Jumamosi, Septemba 20, 2025, saa 9:30 usiku akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rabinisia, jijini Dar es Salaam.

Dk Munga alizaliwa Machi 6, 1955, katika Kijiji cha Tewe wilayani Lushoto, mkoani Tanga, akiwa mtoto wa saba kati ya watoto tisa.

Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Tewe mwaka 1961 hadi 1967. Elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Old Moshi na Tambaza 1969–1971, kisha akajiunga na Chuo cha Theolojia Makumira 1982–1984.

Baadaye alikwenda Sweden kuendelea na masomo na akapata Shahada ya Uzamivu katika Theolojia.

Alifunga ndoa na Aneth Magawa, Aprili 6, 1986, katika Kanisa la KKKT lililoko Maramba.

Askofu Munga amehudumu Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, mwaka 2001 hadi 2022.