Bajana ataja yatakayoibeba JKT Tanzania

KIUNGO wa JKT Tanzania, Sospeter Bajana amesema kikosi hicho kitafanya vyema msimu huu, kwa sababu kuu mbili, falsafa ya Kocha Ahmad Ally na ubora wa mastaa.

Bajana ambaye ameitumikia Azam kwa kipindi cha miaka 15, huu unakuwa msimu wake wa kwanza JKT Tanzania, akiwa amesaini mkataba wa miaka miwili.

JKT Tanzania iliyoanza vyema Ligi Kuu Bara msimu huu, tayari imecheza mechi mbili zote ugenini ikianza na sare ya bao 1-1 dhidi ya Mashujaa, kisha ikaichapa Coastal Union mabao 2-1.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bajana alisema falsafa ya kocha wa JKT ni ya tofauti hali iliyoifanya timu hiyo kubadilika na kucheza soka la kuvutia.

“Tutarajie mengi mazuri kutoka JKT, kwa sababu ni timu yenye ushindani mkubwa, ndiyo maana unaona katika michezo ya mwanzoni tu inapata matokeo mazuri, kwetu ni mwanzo mzuri na lazima nipongeze hesabu za kocha.

“Wachezaji wenye uzoefu wananifurahisha, naona kabisa tutafika mbali.”

Kuhusu kutoonekana kwake katika mechi yoyote kati ya ilizocheza JKT Tanzania, Bajana alisema: “Nitaonekana uwanjani hivi karibuni, ligi ndiyo kwanza imeanza, watu wasijali, ila jambo la muhimu ni mafanikio ya timu kwanza.”

Oktoba Mosi mwaka huu, maafande hao watarejea nyumbani kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Ishamuhyo, jijini Dar kucheza dhidi ya Azam FC ukiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, huku rekodi zikionesha mara ya mwisho kukutana hapo matoko yalikuwa 0-0.