ALIYEKUWA beki wa kushoto wa Simba, Valentin Nouma anakaribia kujiunga na timu ya CI Kamsar ya Guinea, baada ya nyota huyo raia wa Burkina Faso kuondoka Msimbazi alikotumikia kwa msimu mmoja tu.
Nouma alijiunga na Simba, Julai 7, 2024 akitokea FC Saint Eloi Lupopo ya DR Congo kwa mkataba wa miaka mitatu, lakini alifikia makubaliano ya kutoendelea na timu hiyo Julai 12, 2025 kutokana na kutopata nafasi ya kucheza zaidi.
Sababu za kufikia makubaliano ya pande mbili ya kusitisha mkataba na Simba, ni kutokana na kushindwa kupenya mara kwa mara mbele ya aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, ambaye pia ameondoka na kujiunga na Yanga.
Taarifa kutoka Guinea zinaeleza nyota huyo anakaribia kujiunga na CI Kamsar, huku ikielezwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Burkina Faso, Kamou Malo anayeifundisha kwa sasa kikosi hicho ndiye anayemshawishi ili kwenda kuungana naye.
Malo aliyekifundisha kikosi hicho cha taifa kuanzia Julai 24, 2019 hadi Februari 1, 2022, inadaiwa amewasiliana na nyota huyo akimuhitaji, baada ya kuzichezea pia timu mbalimbali zikiwamo za Rahimo na AS Douanes zote kutoka kwao Burkina Faso.
Licha ya kusifika kwa uwezo na uzoefu mkubwa alionao wa kuzuia na kutengeneza mashambulizi, Nouma alishindwa kuwika Msimbazi, jambo lililomfanya kusitisha mkataba wake ili apate timu itakayompa nafasi ya kucheza.
Katika hatua nyingine kiungo wa zamani wa Simba, Debora Mavambo baada ya kuachana na timu hiyo aliyoitumikia kwa msimu mmoja tangu ajiunge nayo Julai 6, 2024, sasa anakaribia kujiunga na Asswehly ya Libya kwa mkataba wa miaka miwili.
Mavambo aliyejiunga na Simba akitokea Mutondo Stars ya Zambia na kufunga bao moja la Ligi Kuu Bara huku akitabiriwa makubwa, alishindwa kuwika na kikosi hicho na sasa anakaribia kujiunga na Asswehly inayofundishwa na kocha Zoran Maki.
Zoran mwenye uraia pacha wa Serbia na Ureno, aliwahi kuifundisha Simba kuanzia Juni 28, 2022, akichukua nafasi ya Pablo Franco raia wa Hispania, ingawa aliondoka Septemba 6, 2022, baada ya kufikia makubaliano ya kusitishiana mkataba wake.
Awali, ilielezwa Mavambo angejiunga na kikosi cha Singida Black Stars ambacho kilionyesha nia ya kumuhitaji baada tu ya kuachana na Simba, japo dili hilo lilishindwa kukamilika na kuamua kutafuta changamoto sehemu nyingine nje ya Tanzania.
Vyanzo mbalimbali kutoka Libya, vinaeleza nyota huyo alitakiwa kujiunga na kikosi hicho tangu mwanzo mwa Septemba 2025, baada kuachana na Simba, ila kilichokwamisha ni kutokana na kesi aliyokuwa nayo ya kusaini timu mbili kwa wakati mmoja.
Inaelezwa, baada ya kusaini mkataba na Asswehly ya Libya, nyota huyo alisaini mkataba mwingine na Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia, jambo lililomuingiza katika utata mkubwa wa kimkataba, japo kwa sasa timu hizo zimefikia makubaliano.
Etoile anayocheza aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Azam, Alassane Diao raia wa Senegal, inaelezwa viongozi wa timu hiyo wamekubali kuachana na Mavambo na sasa kiungo huyo ametua Libya ili kukamilisha taratibu za kujiunga na kikosi hicho.