Tanga. Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema moja ya ahadi kubwa za chama hicho katika ilani ya uchaguzi 2025-2030 ni kujenga upya uwanja wa ndege wa Tanga na kuufanya wa kisasa wenye hadhi ya kimataifa.
Akizungumza leo Jumatano Septemba 24, 2025 baada ya kuwasili jijini Tanga, Wasira amesema uwanja huo ulikuwa na historia ya kipekee lakini kwa sasa umedorora, hivyo CCM imedhamiria kuuendeleza ili kurudisha hadhi yake na kuongeza fursa za kiuchumi na kibiashara kwa wananchi wa mkoa huo.
“Zamani tulikuwa tunakuja Tanga na ndege za East Africa, lakini sasa uwanja umedhoofika. Sasa tumedhamiria kuurudisha ubora wake. Baada ya ukarabati ndege za abiria zitatua Tanga na kutakuwa na taa za kisasa kuhakikisha unakuwa uwanja wa kimataifa,” amesema.
Mbali na uwanja huo, amesema ilani mpya ya CCM pia inalenga kulipendezesha Jiji la Tanga kwa kuweka angalau taa kubwa 100 za barabarani ili kuongeza mwanga na usalama kwa wananchi.
Hata hivyo, Wasira amesema kazi kubwa iliyo mbele ya wanachama na wapenzi wa chama hicho ni kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025 na kuwashawishi wengine kufanya hivyo ili kuihakikishia dunia kuwa Watanzania wako tayari kwa uchaguzi mkuu.
“Dunia inataka kuona kama watu wanapiga kura au hawapigi. Nina imani wananchi wa Tanga mtajitokeza kwa wingi Oktoba 29 kumchagua mgombea urais wetu Dk Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea ubunge na udiwani wa CCM,” amesema.
Vilevile, amesema CCM ina nafasi kubwa ya kushinda kutokana na historia yake ya kutekeleza ahadi, akitolea mfano mradi wa Bandari ya Tanga, vituo vya afya, shule na usambazaji wa maji safi.