Chaumma kubinafsisha sekta ya maji, kujenga viwanda vya jipsamu

Same. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devota Minja ameahidi endapo chama hicho kitapewa ridhaa ya kuingia madarakani, kitaibua mageuzi makubwa katika sekta ya maji kwa kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi kwa Watanzania wote.

Akihutubia leo Jumatano Septemba 24, 2025 katika Kata ya Makanya, Wilaya ya Same Magharibi, Minja amesema Chaumma itabinafsisha sekta ya maji ili kila mwananchi anufaike na huduma hiyo.

Amefafanua kuwa serikali ya chama hicho itahakikisha vyanzo vya maji vilivyopo ardhini vinachimbwa na kuunganishwa kwenye mtandao wa maji utakaoifikia kila kaya.

“Serikali inayokusanya kodi za wananchi inashindwa nini kuchimba maji mengi kwa ajili ya Watanzania? Wapo watu binafsi wamefanikiwa kuchimba na kupata maji, kwa nini Serikali ishindwe? Chaumma tukipewa ridhaa, tutahakikisha kila Mtanzania hapati taabu ya maji,” amesema Minja.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali yao haitategemea mito na mabwawa yanayokauka, bali itaunda mtandao wa kudumu wa maji, akitolea mfano taifa la Misri ambalo limefanikiwa kubadilisha mazingira yake kuwa ya kijani kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji.

Sambamba na hilo, Minja ameahidi kuhakikisha rasilimali ya mawe ya jipsamu yanayopatikana Same yanawanufaisha wakazi wa eneo hilo. Ameeleza kuwa serikali ya Chaumma itahakikisha viwanda vya kuchakata jipsamu vinajengwa ndani ya Same ili kuongeza ajira na kuchochea uchumi wa eneo hilo.

“Tunataka jipsamu lichakatwe hapa hapa, liuzwe hapa na watu wetu wanufaike moja kwa moja. Tukijenga viwanda, mnyororo wa kiuchumi utafaidisha wachimbaji, wafanyakazi, mama lishe, bodaboda na Serikali kwa ujumla,” amesema.

Minja pia ameeleza mikakati mingine ya chama hicho ikiwamo ya ujenzi wa miundombinu, vituo vya afya katika kila kata, ajira kwa vijana na bima ya afya kwa wote.

Amesisitiza kuwa wakazi wa Kilimanjaro watanufaika zaidi iwapo chama hicho kitaingia madarakani na akawataka kuchagua wagombea wa Chaumma kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Same Magharibi, Gervas Mgonja amesema kata 20 za jimbo hilo zinahitaji kiongozi atakayejikita katika kutatua changamoto za wananchi kama uhaba wa vituo vya afya na vyumba vya madarasa.

“Tunayo changamoto ya vituo vya afya na miundombinu chakavu ya shule. Nikiwa mbunge wenu tutajenga vituo vipya na kuhakikisha kunakuwa na majenereta ya dharura pale umeme unapokatika. Nawaomba mnichague mimi sambamba na Salum Mwalimu awe rais wetu,” amesema Mgonja.