Dk Biteko ataja faida nchi za Afrika kuwekeza kwenye elimu

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko ametaja faida zitakazopatikana kwa nchi za Afrika kuwekeza kwenye elimu bora, ikiwemo kuwa na mifumo thabiti ya kidijitali itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo kwenye mataifa hayo, kulingana na mazingira.

Dk Biteko ameitaja faida nyingine ya kuwekeza kwenye sekta hiyo ni kutatua changamoto   ya ukosefu wa elimu bora maeneo ya vijijini.

Ameyasema hayo leo Septemba 24, 2025 katika mkutano wa tano wa kimataifa wa ubora wa elimu ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania TenMeT.


“Tukiwekeza kwenye elimu, tutatatua changamoto ya ukosefu wa elimu bora maeneo ya vijijini, hadi kufikia 2030 Afrika inahitaji walimu milioni 17 ili kuwa na elimu bora ya msingi na sekondari, ambayo ni nyenzo ya kuwapatia wanafunzi kilicho bora,”amesema.

Amesema ni lazima ifike mahali nchi za Afrika iondokane na dhana ya utegemezi wa misaada kwenye sekta ya elimu, kwani kila anayetoa msaada matamanio yake anayepatiwa akue na kujitegemea hivyo ni lazima kila nchi iongeze rasilimali fedha kwenye sekta ya elimu.

Dk Biteko amezitaka nchi za Afrika kufikia matakwa ya utekelezaji wa kuelekeza kwenye sekta ya elimu asilimia   20 ya bajeti ya nchi.


“Katika kutekeleza hili, Tanzania tumepiga hatua kwenye kutenga na kutumia rasilimali za ndani na kuwekeza zaidi kwenye sekta ya elimu.”

“Tumeongeza  bajeti ya Wizara ya Elimu kutoka Sh4.7 trilioni  mwaka 2021 hadi Sh6.6 trilioni  mwaka 2025 na hii ni kiashiria moja wapo kwamba tumeamua kuweka rasilimali  nyingi kwenye elimu ya watoto wetu,”amesema.

Amesema sekta ya elimu katika nchi za Afrika bado ipo nyuma hivyo kunahitajika kuwa na nguvu kuondokana na changamoto zilizopo.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amesema Serikali inaendelea kuboresha sekta ya elimu, akisisitiza elimu inayotolewa nchini ina viwango vya kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitaifa wa TenMeT, Martha Makala amesema mkutano huo una dhamira ya kuimarisha mifumo ya uwekezaji, kukuza uhamasishaji wa rasilimali za ndani kwa elimu jumuishi na endelevu barani Afrika.

Amesema mkutano huo utatoa mbinu ya namna ya kuboresha sera za elimu na kuja na mipango ya kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa na uwekezaji wa uhakika.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya  TenMet, Simon Nanyaro amesema hadi kufikia mwaka 2024 watoto milioni 251 duniani wapo nje ya mfumo wa elimu  na miongoni mwao milioni 100 wapo nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amesema katika sekta ya elimu Tanzania imekuwa ikipiga hatua hasa katika kubadili mitaala ya elimu, ujenzi wa miundombinu ya kufundishia, ujenzi wa shule za sayansi na kuajiri walimu hatua ambayo inaonyesha namna sekta hiyo inavyopewa kipaumbele.