Dk Mwinyi aahidi kuondoa utitiri wa kodi, kupanua wigo wa mikopo

Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amewahakikishia wafanyabiashara ambao hawajapata mkopo unaotolewa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), watapata endapo akipata ridhaa ya kuiongoza tena Zanzibar.

Pia, amesema watapunguza utitiri wa kodi ili waweze kufanya biashara zao kwa tija.

Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 24, 2025 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Chake Chake lililopo wilaya ya Chakehake Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni sehemu ya kampeni zake za kuusaka tena urais kwa kufanya mikutano ya hadhara na kukutana na makundi mbalimbali.

“Ninawahakikishieni kwamba wale ambao hawajapata mkopo wataweza kupata safari hii, lakini wale ambao wamepata wakarejesha watakapopata tena watapata kiwango kikubwa zaidi kwa sababu watakuwa wameonyesha uwezo wao wa kurejesha mikopo wanayoipata,” amesema.

Amesema Serikali ina mikopo aina mbili wa Serikali kuu na inayotokana na mabaraza ya miji na kwa sasa imeunganishwa pamoja kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) ili kuwafikia zaidi wananchi.

Dk Mwinyi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, amesema Serikali itafanya utaratibu wa kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi chache kadri itakavyowezekana.

“Nikisema chache maana yake kusiwe na misururu ya kodi kama bandarini iwe moja na hapa mnapofanya biashara iwe moja na hapo kodi zisichanganywe ziwe kodi ndogo iwe kodi ya kukodi kibaraza na ya usafi,”amesema.

Abdallah Bakari Mohammed ambaye ni mfanyabiashara wa soko la ChakeChake amesema soko hilo ni la zamani tangu kujengwa kwake lina miaka zaidi ya 100.

“Mvua ikinyesha wafanyabiashara wa mbogamboga wananyeshewa tunaomba tuboreshewe soko letu la Chake Chake,”amesema.

Mfanyabiashara huyo amesema soko hilo lina changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa vyoo na maji.