Mbeya. Wananchi Kata ya Ilomba Mkoa wa Mbeya, wamemtaka mgombea ubunge Uyole, Dk Tulia Ackson kuondoa adha ya maji, ujenzi wa kituo cha afya na vumbi kwenye barabara za mitaa huku naye akisema kero zao atazifanyia kazi akishinda uchaguzi mkuu.
Awali akiomba kura za Rais na wabunge na madiwani kwa wananchi, Mzee wa Mila, Chifu Adamson Kipingu amesema wakati wa porojo umepita sasa wanahitaji maendeleo.
Mkazi wa Ituha Selina Hamis, amesema ili kuhakikisha mgombea nafasi ya Rais na ubunge likiwepo la Uyole wanapata kura za kishindo kama wanawake na makundi maalumu kazi ni moja kusaka kura na kutiki Oktoba mwaka huu.
“Tumeona maendeleo ya Mbeya Mjini nasi huku Uyole tunahitaji tumekosa kwa miaka mingi hususani barabara, maji na ukosefu wa kituo cha afya,” amesema.
Amesema kimsingi wameona utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020/2025 sasa wanampa kibarua mgombea ubunge Uyole Dk Tulia akipata ridhaa kuanza na kipaumbele cha barabara, maji na ujenzi wa kituo cha afya Kata ya Ilomba ikiwa ni sehemu ya kutekeleza ilani ya uchaguzi 2025,2030.
Akiomba kura kwa wananchi wa Kata ya Ilomba, Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Mbeya, Philimon Mng’on’go amesema anaona jinsi Uyole itakavyo kimbia kimaendeleo, lakini tunajua kuna upinzani tuombe Oktoba 29, 2025 wampigie kura mgombea ubunge Uyole Dk Tulia na Rais Samia Suluhu Hassan.
“CCM tunahitaji ushindi wa heshima kina mama, kina baba wakati ukifika jitokezeni kupiga kura za heshima za Rais Samia na Dk Tulia kama kurejesha shukrani ya maendeleo yaliyoletwa kwa miaka mitano, “amesema.
Mgombea udiwani Kata ya Ilimba, Noah Mwakisu amesema kauli hizo za wananchi kupigia kura CCM ni kutokana na maendeleo yaliyoletwa na Serikali kipindi cha miaka mitano.
Pia, ameomba kutatuliwa changamoto ya ubovu wa barabara,maji na ujenzi wa kituo cha afya ili kusogeza huduma jirani hususani kwa wakinamama wajawazito.
“Kata yetu ina wananchi 40 ,000 lakini hatuna kituo cha afya, huduma ya maji safi ya uhakika na barabara zetu ni vumbi ombi letu Serikali ilione hilo na kusisitiza wananchi kupiga kura za kishindo Oktoba mwaka huu ili maendeleo kufikiwa na miradi ,”amesema.
Dk Tulia amewaondoa hofu wananchi na kwamba CCM wamejipanga kuleta maendeleo Uyole.
“Akija mtu akikupa habari za Dk Tulia waelezeni tumeishi naye, lakini wana Ilomba mmeona kazi tulizofanya CCM Uyole tumejipanga,”amesema.
Amesema mwakani kuna wanafunzi watajiunga kidato cha kwanza na Serikali imeweka mazingira mazuri na wezeshi hakuna changamoto ya madawati, madarasa.
Amesema mbali na uwekezaji wa Serikali sekta ya elimu kama mgombea ubunge wa kujiongeza ifikapo Januari mwaka 2026 , watoto walio chaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika kaya zisizojiweza watapewa sare za na mahitaji mengine bure lengo watimize ndoto zao za kupata elimu bora.
Amesema Serikali itaendelea kuboesha miundombinu hususani ujenzi wa vituo vya afya ikiwepo utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020/2025 ya ujenzi wa miundombinu ya jengo la ghorofa katika Hospitali ya Rufaa Kanda kitengo cha wazazi Meta kwa gharamu ya Sh11 bilioni ambayo imeanza kutoa huduma.
“Lakini pia tunakuja na utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote ambayo itaanza hivi karibuni sambamba na yeye binafsi kuendeleza kutoa bima za afya kwa Kata 13 za Jimbo la Uyole,”amesema.
Amesema wana Uyole wana bahati kuna ujio wa mradi wa maji Mto Simba sambamba na utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa chanzo cha mto Kiwila Wilaya ya Rungwe.
“Lakini pia niwahakikishie kero ya barabara za mitaa zitatatulia kazi yenu sasa ni kuchagua mafiga matatu Oktoba 29, mwaka huu hususani mgombea urais, wabunge na madiwani,” amesema.