Hamad: Wananchi wanahitaji chakula zaidi na si Katiba

Unguja. Mgombea urais wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohamed amesema chama chake kinahitaji kuwaendeleza wananchi kwa kuhakikisha wanapata chakula cha kutosha kwanza ili wawe na nguvu za kushiriki shughuli za uzalishaji na utafiti wa rasilimali za nchi, na si Katiba mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Septemba 24, 2025, katika mkutano uliofanyika Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Hamad amesema kilio kikubwa cha wananchi si Katiba mpya, bali ni upatikanaji wa chakula.

“Wananchi wanataka kushiba na si Katiba, kwa sababu hiyo haina uwezo wa kumlisha mtu. Ndiyo maana chama hiki kinahitaji kumuendeleza mwananchi mmoja mmoja,” amesema.

Amesema iwapo ADC itapatiwa  ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, ndani ya mwaka mmoja wakulima wote watapatiwa pembejeo bure na kilo moja ya mchele haitazidi Sh1,500.

Aidha, Hamad amesema chama chake hakifanyi kampeni kwa mtindo wa majukwaa ya hadhara, bali kimeamua kutumia njia za kidijitali kwa kuwa wananchi wanahitaji matokeo ya vitendo badala ya maneno.

Akizungumzia sekta ya elimu, amesema mfumo uliopo hauendani na mahitaji ya sasa ya Taifa, hivyo ADC ikichaguliwa itafanya tafiti na kuwapeleka masomoni wanafunzi kulingana na uhitaji wa wataalamu.

Kwa upande wa usalama wa chakula, Hamad amesema Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) vitapewa jukumu la kuzalisha mbegu ili kukabiliana na uhaba wa chakula.

Wananchama na wapenzi wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) waliohudhuria katika mkutano wa waandishi wa habari. Picha na Zuleikha Fatawi



Pia, amesema ADC imepanga kuongeza mshahara wa kima cha chini hadi Sh600,000 kwa lengo la kutoa mizani bure ili kudhibiti mfumuko wa bei, kujenga viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya mwani na kuifanya Zanzibar kuwa soko kuu la karafuu.

Katika hatua nyingine, mgombea urais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania wa chama hicho,Wilson Elias akizungumza na Mwananchi leo, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi Jumatano Oktoba 29, 2025 kwenda kupiga kura.

Elias amesema ADC ina imani kwamba, uchaguzi huo utafanyika kwa uhuru na haki.

“Tunaimani uchaguzi huu utafanyika kwa uhuru na haki kwa sababu tumefanya mazungumzo ya mara kwa mara na viongozi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhusiana na hili, nao wametuhakikishia na wametutoa wasiwasi na sisi tunaamini itakuwa hivyo,” amesema mgombea urais huyo.

Amesema ili hali iwe shwari, anawasihi Watanzania kufuata sheria na maelekezo ya tume.