Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemteua Oscar Mirambo kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo akichukua nafasi ya Kidao Wilfred ambaye mkataba wake unafikia tamati Septemba 30 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa leo Septemba 24, 2025 na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo, imesema: “Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemteua Oscar Mirambo kuwa Kaimu Katibu Mkuu.
“Uteuzi wa Mirambo ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, utaanza rasmi tarehe 1 Oktoba 2025.
“Mirambo anachukua nafasi ya Kidao Wilfred ambaye mkataba wake unamalizika tarehe 30 Septemba 2025.”
Mirambo ana uzoefu mkubwa wa mpira wa miguu alioupata kwa kucheza, kufundisha na kuongoza kwa nyakati tofauti.

Amewahi kuwa mchezaji katika timu ya Pallsons ya Arusha, baadaye akageukia ukocha ambapo jina lake lilianza kuwa maarufu alipokuwa akiinoa timu ya Shule ya Sekondari Makongo ambayo ilikuwa kituo cha kukuza soka kwa vijana.
Kisha aliingia katika ukocha wa program za vijana za TFF hadi kuwa Kocha Msaidizi na baadaye Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 maarufu Serengeti Boys.

Mirambo aliiongoza Serengeti Boys katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo (AFCON U17) ambapo iliishia hatua ya makundi.
Mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, nafasi ambayo anahudumu hadi leo hii.
Mirambo pia ni Mkufunzi wa Makocha wa anayetambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF) na ana leseni ya juu ya ukocha ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA)

Mwezi uliopita aliteuliwa kuwa miongoni mwa Maofisa wa Idara ya Ufundi ya CAF katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024.
Kuondoka kwa Kidao kunahitimisha miaka nane ya utumishi wake katika nafasi hiyo aliyoitumikia tangu Agosti, 2017.

Kabla ya nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu, Kidao alihudumu katika nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA).