Njombe. Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omary amewataka madaktari bingwa waliofika mkoani humo kutoa huduma za kibingwa, kuwapa ujuzi madaktari wa eneo husika ili uwe msaada endelevu.
Zaidi ya madaktari bingwa 36 wanaotibu magonjwa mbalimbali wamefika mkoani Njombe kwa ajili ya kutibu wagonjwa mbalimbali, ambapo wametawanywa katika halmashauri zote za sita za mkoa huo.
Ombi hilo amelitoa leo Septemba 24,2025, wakati akizungumza na madaktari bingwa wanaotoa huduma katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Njombe.
Amesema hiyo ni awamu ya nne ya madaktari hao kutoa huduma za kibingwa mkoani humo, ikiwa ni kwa ufadhili wa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwasaidia wananchi ambao hawawezi kumudu gharama za kufuata huduma za kibingwa katika hospitali za kubwa.
Amesema madaktari hao bingwa wanapofika katika maeneo mbalimbali hapa nchini huwa wanashirikiana na wenyeji wanaowakuta katika utoaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi.
Amesema hivyo hawana budi kubadilishana uzoefu na kuacha ujuzi kwa madaktari watakaowakuta ili nao waweze kutoa msaada kwa wananchi watakapoondoka.
“Mnapokuja huku pia mnashirikiana na madaktari ambao wapo huku na mtakaposhirikiana kwa ukaribu mnasikilizana na kupeana uzoefu na kubadilishana ujuzi,” amesema Omary.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Juma Mfanga amesema mkoa huo una vituo vya kutoa huduma 376 huku hospitali zikiwa 18 na saba ni za Serikali pia kukiwa na vituo vya afya zaidi ya 50 na zahanati 303.
“Madaktari bingwa 36 waliofika watahudumia katika halmashauri zote sita za Mkoa wa Njombe na huduma za kibingwa zimesogezwa karibu na wananchi.”
Mratibu wa huduma za matibabu hayo, maarufu ‘Madaktari wa Samia’ Mkoa wa Njombe, Paskalina Andrew amesema wanajua kuwa madaktari bingwa wanafanya kazi nzuri ya kusaidia wananchi lakini wanapofika kwenye vituo waweze kushirikiana na wenyeji wao.
“Ni kweli mgeni apokelewe vizuri lakini tunaomba na nyinyi mtoe ushirikiano kwa wale tutakaowakuta kwenye vituo,” amesema Andrew.
Mmoja ya madaktari bingwa hao Dk Monica Mboka amewaomba wananchi kujitokeza kupatiwa huduma za kibingwa kwani ni nafasi pekee ambayo wanaweza kuitumia.
“Tunawaalika wananchi wote hata kutoka mikoa jirani waje kupata huduma hizi kwani ni adimu na nafuu,” amesema Mboka.
Baadhi ya wananchi waliofika kupatiwa huduma akiwemo Shime Gwishi ameishukuru Serikali kwa kuletewa madaktari bingwa karibu nao kwani, uwepo wao utasaidia kwa kuwa wengi wao hawana uwezo wa kufuata huduma hizo katika hospitali kubwa.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuwaleta madaktari hawa maana wengi wenu hatuna uwezo wa kumudu hizi gharama,” amesema Gwishi.