Mambo ‘yametiki’ Simba, kocha mpya huyu hapa

KUNA mambo kadhaa yapo hapa kipindi hiki ambacho mabosi wa Simba wanaendelea kusaka kocha atakayerithi mikoba ya Fadlu Davids, huku mezani jina la kocha mmoja kutoka Madagascar likipigiwa kura nyingi, baada ya kubainika wamekutana na ugumu wa kumng’oa Miguel Gamondi Singida Black Stars.

Katika mambo ambayo Simba inakabiliana nayo kipindi hiki kabla ya kufika wiki ijayo ambayo huenda akatangazwa kocha mpya, timu hiyo ina mechi mbili za mashindano tofauti.

Alhamisi, inakabiliana na Fountain Gate katika Ligi Kuu Bara, kisha Jumapili itacheza dhidi ya Gaborone United ukiwa ni mchezo wa marudiano hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mechi hizi zote zitachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.

Wakati mchakato wa kumpata mrithi wa Fadlu ukiendelea, hivi sasa Simba iko na kocha wa muda, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye pia anakinoa kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars. Morocco atakuwa akifanya kazi na Seleman Matola ambaye ni kocha msaidizi wa kikosi hicho.

Morocco amechukuliwa na Simba kwa ajili ya mchezo dhidi ya Gaborone United utakaofanyika Septemba 28, mwaka huu. Kumbuka Simba inaongoza 1-0, ushindi ilioupata ugenini wikiendi iliyopita.

Wakati Morocco akichukuliwa kwa jukumu hilo, Matola ataanzisha mwendo kucheza dhidi ya Fountain Gate, mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Alhamisi.

Mwanaspoti linafahamu, Simba ilijua mapema Fadlu hatakuwa na muda mrefu na kikosi hicho, lakini ikawa inasikilizia kwani katika mkataba wa mwaka mmoja uliobaki kulikuwa na kipengele cha upande utakaovunja mkataba huo, utalazimika kulipa mishahara ya miezi mitatu.

Mapema jana, Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliwasili jijini Dar es Salaam, tayari kwa kupokea jukumu jipya la kuifundisha Simba kwa muda na siku hiyo hiyo alitarajia kuanza kazi rasmi ya kusimamia mazoezi, huku mwenyewe akifunguka kazi atakayokutana nayo.

Morocco aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea nyumbani kwake Zanzibar, ikiwa ni siku moja tangu usiku wa Septemba 22, 2025 atangazwe kuchukua majukumu hayo baada ya kuondoka kwa Fadlu.

Akizungumza mara baada ya kuwasili, Morocco alisema haikuwa rahisi kukubali jukumu hilo lakini ametaja weledi ndio umemfanya akubaliane na ajira hiyo ya muda.

“Nimefika salama namshukuru Mungu, ninachoweza kusema nakwenda kukabiliana na changamoto nzuri, lakini ina ugumu wake,” alisema Morocco ambaye amewahi kuzifundisha klabu za Namungo, Geita na Coastal Union.

“Haikuwa rahisi kukubalina na hili jukumu, unajua mimi bado ni kocha wa timu ya taifa, lakini baada ya kuzungumza na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maana wao ndio waajiri wangu walikubali kunipa hiyo nafasi.

“Nimetanguliza weledi kwenye kuamua hili, nakwenda Simba ni timu kubwa, nahitajika kwenda kutuliza presha ya wafuasi wake wengi ambao wanatarajia kuona timu yao inatulia.

“Nakwenda kujiunga na timu ambayo sikufanya usajili na ipo kwenye mashindano, lakini pia haikuwa na utulivu mkubwa, nampongeza kocha aliyetangulia Fadlu (Davids) ni rafiki yangu amefanya kazi yake nzuri na ameondoka, nadhani ni hatua ya kuanzia hapa alipoishia na kwenda mbele.”

Morocco alisema anafahamu ametua Simba kwa ajili ya kuchukua nafasi ya muda mfupi, wakati klabu ikisaka kocha mpya atakayekuja kukiongoza kikosi hicho msimu huu wa 2025-2026.

“Nimetua Simba kuja kuchukua nafasi ya muda kuifundisha baada ya Fadlu kusitisha ajira yake, hivyo nipo kwa ajili ya mechi chache zijazo hasa kimataifa,” alisema.

Kuhusu uamuzi wa kumchukua Morocco, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori alisema: “Hemed Morocco tumemchukua kwa ajili ya kusimamia mechi ya Ligi ya Mabingwa, kwa sababu lazima uwe na leseni ya CAF A kuweza kusimamia, Matola ana CAF A lakini amepata kadi nyekundu, hawezi kusimama Jumapili.

“Wakati tunatafuta kocha wa haraka, ilikuwa ni ngumu kwenda kumchukua kocha wa klabu nyingine kwa ajili ya kusimamia tu mechi ya Jumapili.

Akizungumzia mchakato wa kumpata mrithi wa Fadlu, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Tunafanya mchakato kwa haraka hadi kufikia wiki ijayo tuwe tumempata kocha na kuunda benchi lote la ufundi, viongozi hawalali tangu juzi kuhakikisha wanampata kocha bora atakayekuja kufanya kazi na Simba SC.

“Wakati huo tukitafuta kocha, tuna mechi mbili hapa za haraka haraka, tuna mechi tarehe 25 na tarehe 28. Mechi ya ligi kuu dhidi ya Fountain Gate hii atasimama Seleman Matola, tuna imani naye na uzoefu wa kutosha, pia ana vigezo vya kusimamia klabu zote zinazoshiriki ligi kuu akiwa kocha mkuu.

“Kwa upande wa Hemed Morocco, licha ya kwamba ataanza kuisimamia Simba hivi sasa kuanzia mazoezini lakini kazi yake maalum ipo katika mchezo wa tarehe 28 kuhakikisha Simba anamtoa Gaborone na anakwenda hatua inayofuata. Makocha hao wataanza vibarua vyao rasmi leo (jana).”

Baada ya Fadlu kuondoka ghafla, jina la kwanza ambalo lilikuwepo mezani kwa mabosi wa Simba ni la Miguel Gamondi raia wa Argentina, kocha aliyewahi kuinoa Yanga lakini sasa yuko Singida Black Stars. Simba ilichofanya ni kama ilivyowahi kukifanya Yanga alipoondoka Sead Ramovic katikati ya msimu uliopita.

Taarifa zililiambia Mwanaspoti: “Simba ilipoicheki tu Singida ilikutana na mgomo wa ombi hilo, huku mabosi hao wakiwaambia, kwa sasa hawawezi kuwasaidia hilo kwani wanashiriki michuano ya kimataifa.”

Ikumbukwe, wakati Ramovic anaondoka Yanga Februari 2025, ilikwenda kumchukua Miloud Hamdi ambaye siku chache alikuwa ametambulishwa Singida, akatua na kumalizia msimu akishinda Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, kisha akatimkia Ismailia ya Misri.

Simba ikaanza mchakato wa kuzungumza na wanaomsimamia Kocha Benni McCarthy ambaye kwa sasa anaifundisha timu ya Taifa ya Kenya, lakini kifurushi chake kikawa kikubwa, huku akitaka apewe muda, wakati Simba inataka kocha haraka.

Mwanaspoti linafahamu, licha ya makocha wengi kuomba nafasi ya kuifundisha Simba, uongozi wa klabu hiyo upo kwenye mazungumzo na kocha wa timu ya taifa ya Madagascar, Romuald Rakotondrabe, aliyeiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika mwaka huu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti: “Simba inatafuta kocha haraka ambaye atakuja kabla ya mchezo wa marudiano na kuna uwezekano wakamalizana na kocha wa Madagascar.

“Morocco amekuja kwa ajili ya mechi moja pekee ya marudiano dhidi ya Gaborone United, baada ya hapo timu ndiyo itaendelea kufundishwa na huyo kocha mpya ndiyo maana mchakato unafanyika kwa haraka sana.

“Wakati mchakato ukiendelea na ujio wa Morocco, kwa asilimia kubwa Matola atakuwa akitoa msaada wa kukijenga timu kwani amekuwa nayo kwa muda mrefu, hivyo hata kama hatokuwa kwenye benchi Jumapili, lakini katika uwanja wa mazoezi atasaidia pakubwa sana.”

Endapo Simba itamalizana na Kocha Rakotondrabe, basi kibarua chake cha kwanza kinatarajiwa kuwa Oktoba Mosi 2025 dhidi ya Namungo, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Julai Mosi 2025, Rakotondrabe mwenye umri wa miaka 60, aliteuliwa kukiongoza kikosi cha Madagascar kushiriki michuano ya CHAN 2024 na kukifikisha fainali, kikapoteza mbele ya Morocco. Kocha huyo mwenye leseni ya UEFA Pro, amekuwa akipenda kutumia mfumo wa 4-3-3.