Maximo akomalia mastraika KMC | Mwanaspoti

KICHAPO cha bao 1-0 ilichopewa KMC katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Singida Black Stars, kimemuamsha kocha wa timu hiyo, Mbrazili Marcio Maximo akisema changamoto kubwa iliyowagharimu ni katika eneo la safu ya ushambuliaji.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam baada ya mechi hiyo, Maximo alisema eneo la ushambuliaji lilikosa mabao mengi kutokana na nafasi nyingi zilizotengenezwa, japo kitu anachofurahia ni kuona wachezaji jinsi wanavyopambana zaidi.

“Ni hatua kwa hatua kwa sababu wachezaji ni wadogo na wanahitaji kuendelea kukuzwa zaidi katika vipaji vyao, sio suala la usiku mmoja kuona hilo likitokea, ila napata matumaini makubwa kutokana na kile wanachokionyesha,” alisema.

Aidha, Maximo alisema baada ya mechi hiyo amewataka wachezaji kusahau matokeo yaliyopita na badala yake wawekeze nguvu kwa mechi zijazo, kwa sababu huu ni mwanzo na wana safari ndefu ya kurekebisha changamoto zilizojitokeza.

Kichapo hicho kwa KMC ni cha kwanza kwa msimu huu katika Ligi Kuu Bara, baada ya kikosi hicho kuanza vyema kwa ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji Septemba 17, 2025, lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Daruweshi Saliboko katika dakika ya 56.

Hii ni mara ya tatu kwa Maximo kuja Tanzania kufundisha soka, baada ya awali kuwa kocha wa Taifa Stars kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, kisha baada ya hapo akaifundisha pia Yanga 2014, akiwa ni miongoni mwa makocha waliojizoelea umaarufu.

Maximo amerejea nchini akiwa na kumbukumbu nzuri, kwani ndiye kocha wa kwanza pia kuiongoza timu ya taifa ya Taifa Stars kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani (CHAN), iliyofanyika Ivory Coast mwaka 2009.