Mirambo achukua mikoba ya Kidao TFF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemteua Oscar Mirambo kuwa Kaimu Katibu Mkuu akichukua nafasi ya Kidao Wilfred ambaye mkataba wake unafikia tamati Septemba 30 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa leo Septemba 24, 2025 na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo, imesema: “Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemteua Oscar Mirambo kuwa Kaimu Katibu Mkuu.

“Uteuzi wa Mirambo ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, utaanza rasmi tarehe 1 Oktoba 2025.

“Mirambo anachukua nafasi ya Kidao Wilfred ambaye mkataba wake unamalizika tarehe 30 Septemba 2025.”

Kidao anahitimisha utumishi wake katika nafasi hiyo baada ya miaka minane ambapo awali aliteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 akiwa amekaa kwenye kiti hicho kwa mihula mitatu tofauti ya uongozi wa Rais wa TFF, Wallace Karia.