Mke wa Trump anusurika kuanguka, ‘White House’ yataka uchunguzi

New York. Rais wa Marekani, Donald Trump alianza hotuba yake ya dakika 55 katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kuikosoa taasisi hiyo kufuatia hitilafu ya ngazi ya umeme (escalator) iliyokaribia kumuangusha mkewe, Melania Trump.

Rais Trump ambaye jana Jumanne Septemba 23, 2025 amehutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni kama alikuwa amepandwa na hasira kwa tukito ambalo baadaye lilitolewa ufafanuzi na msemaji wa Umoja wa Mataifa.

Ngazi hiyo ya umeme (escalator) ilisimama ghafla wakati Trump na mkewe wakipanda katika jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa alipokuwa akienda kuhutubia taasisi hiyo yenye nchi wanachama 193.

Trump alipokuwa akitoa hotuba yake alitoa tathmini juu ya uwezo wa taasisi ya kimataifa hiyo.


“Kile pekee nilichopata kutoka Umoja wa Mataifa ni ngazi ambayo, ilipokuwa ikipanda, ilisimama katikati kabisa. Kama ‘First Lady’ (Mke wa Rais) asingekuwa na hali nzuri, angeanguka,” alisema Trump akimaanisha mkewe Melania Trump.

Trump aliendela kulaumu; “Haya ni mambo mawili tu niliyopata kutoka Umoja wa Mataifa: ngazi mbaya na ‘teleprompter’ mbaya (Kifaa cha kusaidia kusoma hotuba bila kuangalia chini kwenye karatasi).”

Kufuatia tukiop hilo la ngazi kusimama ghafla kwa sekunde chache, Ikulu ya White House imetoa wito wa uchunguzi kuhusu hitilafu hiyo.

Hata hivyo, msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric ametoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo kwamba hitilafu hiyo imetokana na kitendo cha mpigapicha wa Rais Trump kuwahi mbele ya kiongozi huyo kuchukua picha za kumbukumbu kulifanya aguse sehemu iliyosimamisha ngazi hiyo.


Dujarric alifafanua kwamba mpiga video huyo huenda bila kukusudia aligusha moja ya kifaa cha usalama cha ngazi hiyo na kuifanya isimame ghafla.

Amesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuguswa kwa kifaa cha usalama wa ngazi ambacho kazi yake ni kulinda usalama wa watumiaji wanapoteleza kwa bahati mbaya, kuwasaidia wasianguke kwa kukigusa na kuzima kwa muda.

Tangu Trump aingie madarakani, uhusiano kati ya Marekani na Umoja wa Mataifa umedorora.

Hivi karibuni, Marekani imejiondoa kutoka katika mashirika kadhaa ya UN, yakiwemo Baraza la Haki za Binadamu, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), pamoja na Shirika la Misaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Kati.


Pia, Rais Trump alianza hotuba yake kwa kutangaza kuwa kifaa cha kusaidia kusoma hotuba bila kuangalia chini kwenye karatasi ‘teleprompter’ hakifanyi kazi.

“Sina tatizo kutoa hotuba hii bila teleprompter, kwa sababu teleprompter haifanyi kazi,” alisema, akidai bado ana furaha kuwa ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu.

“Naweza kusema tu kwamba yeyote anayesimamia teleprompter hii yuko kwenye matatizo makubwa,” aliongeza.

Dakika chache baada ya kuanza hotuba yake, Trump alionekana akisoma kutoka kwenye nakala ya hotuba yake iliyochapishwa kwenye karatasi.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.