Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya(33) anayekabiliwa na kesi uhujumu uchumi, anaendelea kusota rumande kwa kufikisha siku 1,000, kutokana na Jamhuri kutokukamilisha upelelezi wa kesi hiyo.
Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Kwa mara ya kwanza, Gasaya alifikishwa mahakamani hapo, Desemba 29, 2022 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili.
Tangu siku hiyo hadi leo, Jumatano Septemba 24, 2025, mshtakiwa huyo, amefikisha siku 1,000, akiwa rumande, kutokana upande wa mashtaka kutokukamilisha upelelezi dhidi ya kesi inayomkabili.
Siku hizo 1,000 ni sawa na miaka miwili, miezi minane na siku 26, ambazo pia ni sawa na miezi 32 na siku 26 akiwa mahabusu mshtakiwa huyo kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokukamilika.
Hata hivyo, leo kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na wakili wa Serikali, Roida Mwakamele aliieleza Mahakama hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo wanaomba tarehe kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Mwakamele baada ya kutoa taarifa hiyo, mshtakiwa aliomba Mahakama ielekeze upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi kwa wakati kutokana na kesi hiyo kuwa ni ya muda mrefu.
Hakimu Magutu baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka na mshtakiwa, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 8, 2025 , kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu.
Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC iliyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.