Mtihani mwingine Ibenge, Folz Bara

LEO Jumatano, Kocha wa Azam, Florent Ibenge na wa Yanga, Romain Folz, wanaanza kibarua cha kuziongoza timu hizo katika Ligi Kuu Bara. Makocha hao wanaingia uwanjani wakiwa wametoka kupata ushindi muhimu ugenini kwenye mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) upande wa ngazi ya klabu.

Azam itaikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 3:00 usiku, kabla ya hapo, saa 1:00 usiku Yanga itakuwa mwenyeji wa Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Yanga ambayo imepata ushindi wa mabao 3-0 ugenini Angola dhidi ya Wiliete kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ni mechi inayoanzisha safari ya zaidi ya miezi minane ya timu hiyo kutetea taji la Ligi Kuu Bara ambalo inalisaka kwa mara ya tano mfululizo.

Kumbukumbu nzuri ya ubabe ambayo Yanga imekuwa nayo dhidi ya Pamba Jiji pindi zikutanapo kwenye Ligi Kuu, hapana shaka unaiweka katika hali nzuri kisaikolojia katika mchezo wa leo kwani imepata ushindi mara zote mbili msimu uliopita ikifunga jumla ya mabao 7-0. Ilianza 4-0 nyumbani, ugenini ikashinda 3-0.

Wakati huo ukiwa ni mchezo wa kwanza wa Yanga Ligi Kuu msimu huu, Pamba Jiji inaingia ikiwa imetoka kupata pointi moja kwa kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Namungo.

Ikiwa itapata ushindi au sare, Yanga itaboresha rekodi yake ya kutopoteza mechi za Ligi Kuu kwa muda mrefu na hadi sasa imeshacheza michezo 20 bila kupoteza ikipata ushindi katika mechi 19 na kutoka sare moja.

Mchezo huo wa leo utachezeshwa na Refa Abdul Wajihi ambaye atasaidiwa na Janeth Balama na Omari Juma huku refa wa akiba akiwa ni Isihaka Mwalile.

“Kila mara tunaangalia kufanya vizuri zaidi. Ni changamoto lakini tupo tayari kwa hilo kuhakikisha linatimia. Kazi yangu ni kupanga wachezaji 11 uwanjani na wengine katika benchi. Namhitaji kila mmoja kutimiza malengo yetu,” alisema Folz.

Kocha wa Pamba Jiji FC, Francis Baraza amesema anafahamu sio rahisi kukabiliana na Yanga lakini timu yake itajitahidi kukabiliana nao.

“Nawapatia wachezaji wangu fursa wakipata nafasi waonyeshe na mimi sina uoga wowote. Timu ikiwa imara na makosa yakipungua, najua mchezo utakuwa mzuri,” alisema Baraza.

Kuanzia saa 3:00 usiku, Azam FC itaikaribisha Mbeya City katika Uwanja wa Azam Complex katika mchezo ambao ni wa kisasi kwa kila upande.

Azam ina kisasi cha kulipa kwa Mbeya City kwa vile timu hiyo msimu uliopita ilisitisha safari yao katika Kombe la Shirikisho (FA) uwanjani hapo hapo.

Kwa upande wa Mbeya City, bila shaka inataka kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 na Azam FC katika mechi ya kilele cha Tamasha lao la Mbeya City Day mwaka huu.