Pacome afanya balaa, Yanga ikianza kibabe Ligi Kuu Bara

YANGA imeanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kwa kishindo ikianzia ilipoishia kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji, tofauti ikiwa ni kuongeza bao moja wakati inamalizia msimu uliopita kwa kuinyuka Simba 2-0 na kubeba ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.

Mechi hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, hakuna shabiki wa Yanga aliyefurahia namna timu hiyo ilivyocheza kipindi cha kwanza licha ya wenyeji hao kutoka na uongozi wa bao 1-0.


Licha ya kucheza vibaya mashabiki walisubiri mpaka dakika ya 45+3 kushangilia bao la kwanza mfungaji akiwa kiungo  mpya Lassine Kouma kwa kichwa akimalizia kona ya Edmund John.

Bao hilo limeifanya Yanga kushusha presha ikimaliza dakika 45 za kwanza kwa utangulizi wa bao hilo.

Kipindi cha pili Yanga ikabadilika ambapo mabadiliko ya wachezaji watano yakianzia dakika 56 yakairudishia ubora timu hiyo na kuanza kutengeneza mashambulizi makali.


Maxi Nzengeli akaipatia Yanga bao la pili dakika ya 61 akimalizia krosi ya beki wake wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akitoa asisti yake ya kwanza kwenye mchezo wa kwanza akianza kikosi cha kwanza.


Nzengeli kwenye mchezo wa kwanza wa ligi msimu uliopita alifunga bao la kwanza kipindi cha kwanza dhidi ya Kagera. Yanga ikaendelea kutawala mchezo ikipata bao la tatu dakika ya 89 kwa kichwa akimalizia krosi ya Pacome Zouzoua.

Hadi mwisho wa mchezo huo Yanga ikatoka na ushindi wa mabao 3-0, ikianza vyema mbio za ubingwa kwa kushika nafasi ya nne nyuma ya JKT Tanzania, Mashujaa na Namungo zenye pointi nne kila moja zikiwa zimecheza mechi mbili kama ilivyokuwa kwa Pamba Jiji iliyoshuka kutoka nafasi ya tisa hadi ya 11.