Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia Padri Jordan Kibiki wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mafinga kwa tuhuma za kutoa taarifa kuwa alitekwa.
Akizungumza Akizungumza leo Jumatano Septemba 24, 2025, Kamanda wa Jeshi la Polisi Iringa, Alan Bukumbi amesema kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, polisi imebainika Padri Kibiki alikuwa anakabiliwa na madeni baada ya kukopa fedha kutoka kwa watu mbalimbali na kushindwa kuzirudisha.
Kamanda huyo amedai padri huyo hakutekwa kama ilivyoripotiwa awali, bali alitoa taarifa za uongo kupitia mtandao wa WhatsApp akidai kuwa ametekwa na kusafirishwa kuelekea Mbeya lakini baada ya uchunguzi wa Polisi, alikutwa akiwa Mbalizi mkoani Mbeya.

Mbali na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limeeleza kufanikisha operesheni ya kuwakamata watuhumiwa watano Juni 2025, akiwemo raia wa Congo Yanick Mbombo Cele Mchungaji wa Kanisa la Ebenezer Restoration Ministry for All Nations tawi la Iringa ambapo mtuhumiwa huyo na wenzake walibainika kuwatapeli waumini kwa madai ya kufanya miujiza ya uponyaji na baada ya makubaliano ya kisheria, magari matatu ya Yanick yalitaifishwa na kulipa faini ya Sh 20 milioni na kuondolewa nchini.

Aidha, Septemba 15, 2025, polisi waliwakamata Mansour Ahmed na Japhet Masunga, wafanyabiashara wa eneo la Mkimbizi mkoani Iringa, wakiwa na dhahabu yenye uzito wa gramu 2,995.74 na thamani ya zaidi ya Sh 755 milioni bila kuwa na vibali halali.

Jeshi la Polisi limesema matukio hayo yanaashiria uwepo wa baadhi ya watu kutumia nafasi za dini na biashara kufanya vitendo kinyume cha sheria, hali inayoweza kuleta taharuki na upotoshaji katika jamii hivyo Wananchi wametakiwa kuwa makini na kutafuta taarifa sahihi badala ya kuamini kila kinachoandikwa kwenye mitandao ya kijamii.