Raia wa China aomba kubadilishiwa mahabusu, Mahakama yamjibu

Dar es Salaam. Raia wa China, Li Hao, anayekabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh752 milioni kwa njia ya udanganyifu, ameiomba Mahakama imbadilishie mahabusu ya Keko na impeleke Segerea ili iwe rahisi kwake kupata mawasiliano kutoka kwa raia wenzake.

Hao, anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh752 milioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka kampuni ya Gain Company Limited, kwa madai kuwa angewapelekea bando za chuma, jambo ambalo alijua kuwa ni uongo.

Mshtakiwa ametoa maombi hayo leo Jumatano Septemba 24, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi yake ya uhujumu uchumi ilipoitwa kutajwa.

Raia huyo wa China amewasilisha ombi hilo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.

Mshtakiwa huyo ameomba mahakama imbadilishie mahabusu ya Keko anapokaa kwa sasa kutokana na kukosa dhamana na imhamishie mahabusu ya Segerea kwa madai kuwa anaamini kuna raia wenzake wa China, hivyo ni rahisi kufanya mawasiliano nao.

Mshtakiwa huyo alidai mahabusu ya Keko hajaona raia wa China na kama wapo sio wengi, hivyo akipelekwa mahabusu ya Segerea itakuwa rahisi kwake kuwasiliana na wenzake ndani ya mahabusu hiyo.

Hakimu Magutu baada ya kusikiliza maombi hayo, alimtaka mshtakiwa kuwasilisha ombi hilo kwa hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini ambaye anasikiliza kesi hiyo.

“Mshtakiwa, ombi lako liwasilishe kwa hakimu anayesikiliza kesi yako ili aweze kulitolea uamuzi kwa sababu kesi yako imeletwa kwangu kwa ajili kutajwa na kuahirishwa” amesema Hakimu Magutu.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Hakimu Magutu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 8, 2025 kwa kutajwa na mshtakiwa amerudishwa kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Awali, kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa Serikali Roida Mwakamele amedai shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea.

Mwakamele amedai, kutokana na hali hiyo anaomba mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Katika kesi ya msingi, Hao anadaiwa kutenda makosa hayo, Januari 2, 2025 katika benki ya CRDB, tawi la Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni,

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa akiwa eneo hilo kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh752 milioni kutoka kampuni ya  Gain Company Limited, kwa madai kuwa angewapelekea bando za chuma, jambo ambalo alijua kuwa ni uongo.

Pia, siku na eneo hilo, mshtakiwa  alitakatika kiasi hicho cha fedha, wakati akijua ni fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa huyo yupo rumande  kwa sababu kosa la utakatishaji fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.