Dar es Salaam. Baada ya changamoto zilizodumu kwa muda mrefu, Serikali ya Tanzania imesema mazungumzo kuhusu mradi wa chuma wa Liganga na makaa ya mawe wa Mchuchuma yamefikia hatua ya uamuzi, huku hoja zilizokuwa zikisababisha ucheleweshaji kama mgawanyo usio sawa wa hisa na masharti ya mikataba yaliyowapendelea zaidi wawekezaji wa kigeni zikishughulikiwa.
Akizungumza leo Jumatano, Septemba 24, 2025, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Serikali na mshirika wake kutoka China, Shudao Investment Group Company Ltd. (SDIG), wako karibu kukamilisha mikataba mipya itakayozindua rasmi miradi hiyo mikubwa.
“Tangu Januari 2025, Serikali imekuwa ikijadiliana na Kampuni ya SDIG kuhusu vipengele vya mkataba ambavyo haikuridhika navyo. Mazungumzo yapo hatua za mwisho na tumeshakubaliana mambo mengi ya msingi,” amesema Profesa Mkumbo.
Amesema miradi hiyo ni sehemu ya mikakati ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikilenga kuzalisha umeme kupitia makaa ya mawe ya Mchuchuma na kuzalisha chuma cha Liganga kitakachopunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje.
“Mara itakapoanza, Liganga itaiweka Tanzania katika nafasi ya nne kwa uzalishaji wa chuma barani Afrika, baada ya Afrika Kusini, Misri na Libya. Hii itapunguza gharama za miundombinu na kuchochea ukuaji wa viwanda vidogo nchini,” amesema waziri huyo.
Mradi huo ulianza kujadiliwa tangu mwaka 1996 chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), lakini ulikwama mara kwa mara kutokana na mikataba isiyo na uwiano.
Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation (SHG) ya China ilipata zabuni mwaka 2011 na kuingia ubia na NDC, lakini utekelezaji ulisimamishwa mwaka 2015 baada ya Serikali kubaini upungufu.
Mwaka 2024, SHG ilinunuliwa na SDIG inayomilikiwa na Serikali ya Jimbo la Sichuan, hatua iliyofufua tena majadiliano yaliyorejea Januari 2025.
Kwa sasa, Serikali imeshakamilisha malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha mradi na eneo lote lipo chini ya umiliki wake.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, miradi ya Liganga na Mchuchuma itachangia ajira, kuongeza mauzo ya nje na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa za chuma.
Serikali pia imehusisha uendelezaji wa miradi hiyo na mageuzi mapana ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
“Mpango huu unalenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje. Katika utekelezaji wa Dira 2050, Serikali itahakikisha biashara ndogo na za kati za Watanzania zinanufaika moja kwa moja na uwekezaji mkubwa kama huu,” amesema Profesa Mkumbo.
Hata hivyo, imeelezwa kwamba kufufuliwa kwa miradi ya Liganga na Mchuchuma ni sehemu ya mpango mpana wa miradi ya kielelezo, inayohama kutoka Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo ya Miaka Mitano (FYDP III 2021/22–2025/26) kuelekea FYDP IV.
Timu ya wataalamu 22 kutoka sekta ya umma na binafsi, chini ya uenyekiti wa Dk John Mduma, imeidhinisha kuendelezwa kwa miradi 12 kati ya 17 inayoendelea.
Baadhi ya miradi iliyokamilika ni Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (MW 2,115), ujenzi wa madaraja makubwa 13 na kiwanda cha sukari cha Mkulazi.
Inayoendelea ni pamoja na Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) yenye vipande vinane, Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) lenye urefu wa kilomita 1,443 ukiwa umefikia asilimia 55 kukamilika, na Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, ambao umefikia asilimia 75.
Miradi mingine ni pamoja na umeme wa maji wa Ruhudji (MW 358, asilimia 6 kukamilika), Rumakali (MW 222, asilimia 7), LNG Lindi (asilimia 6), utafutaji mafuta na gesi Eyasi-Wembere (asilimia 5), Mnazi Bay-Mtwara (asilimia 6), magadi soda Engaruka-Arusha (asilimia 5), Kanda Maalum ya Kiuchumi Bagamoyo (asilimia 5), reli ya kusini kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay (hatua za awali), na mradi wa makaa ya mawe na chuma wa Mchuchuma-Liganga wenyewe.