Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kitengo cha Kudhibiti fedha haramu (FIU) wametiliana saini mkataba wa kubadilishana taarifa nyeti.
Tukio hilo limefanyika ofisi za Takukuru makao makuu Dodoma leo Jumatano Septemba 24, 2025 mkataba ukitajwa kuwa unakwenda kumaliza mapungufu ya kiuchunguzi na muda unaotumika hasa kwenye uchunguzi na utakatishaji fedha.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Crispin Chalamila amesema mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa ikiwa taasisi hiyo haitawashirikisha wadau wengine.
Chalamila amesema Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2023 inataka taasisi zinazotaka kubadilishana taarifa lazima ziwe zimesaini mkataba maalumu na ndiyo maana wameingia mkataba huo.

“Hawa FIU tangu tumeanza kufanya nao kazi tumeona manufaa makubwa, mfano katika kipindi cha 2022 hadi 2025 tulipokea taarifa fiche 47 kutoka kwao na kati ya hizo, 36 tumezifanyia kazi na kuona umuhimu wa kuwa nao,” amesema Chalamila.
Mbali na taarifa hizo, lakini Chalamila amesema wameomba FIU iwapatie taarifa zingine muhimu 141 ili nazo wazifanyie kazi baada ya kuona ipo haja kufanya hivyo na wamekuwa wakishirikiana vema.
Kwa mujibu wa Chalamila, kwa sasa watachukua muda mfupi kufanya uchunguzi kwenye masuala ya matumizi mabaya ya fedha, rushwa na utakatishaji fedha kwa pande zote mbili, kuliko muda ambao walikuwa wakiutumia kabla ya kuingia makubaliano hayo.
Mkurugenzi wa FIU, Majaba Magana amesema Tanzania ilikuwa na upungufu katika maeneo 21 ambayo yaliainishwa kimataifa ambayo yote yalitokana na kutokuwa na mifumo inayosomana.
Magana amesema tangu Juni mwaka huu baada ya Serikali kuagiza kuwe na mifumo ya pamoja inayosomana, hakuna mapungufu tena na pamekuwa na mifumo imara yenye kutoa taarifa sahihi.
Amesema licha ya kufanya kazi za pamoja na Takukuru, lakini wakati wa uingizaji taarifa kulikuwa na mapungufu na makosa ya kibinadamu yalijionyesha hivyo wakaona ipo haja kwenda mbele zaidi.

“Baada ya kusaini makubaliano haya, sasa tunakwenda kuongeza ufanisi na upimaji katika uwajibikaji, lakini tunaboresha taarifa zetu,” amesema Magana.
Awali Mkurugenzi wa Sheria wa FIU, Adam Kilongozi amesema mkataba huo unaohusu kupata taarifa na mambo husika ya kifedha, utadumu kwa miaka mitano.