Trump ‘aikomalia’ Hamas, viongozi wengine wataka taifa huru la Palestina

Dar es Salaam. Wakati Rais Donald Trump akisema kutambua taifa la Palestina ni “zawadi kwa Hamas,” viongozi wengine, akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, wameunga mkono kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina.

Viongozi hao wametoa maoni yao wakati wakihutubia kwa nyakati tofauti mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, huku Rais wa Indonesia, Prabowo Subianto, akihutubia kwa mara ya kwanza mkutano huo tangu aingie madarakani. Alinukuliwa akisema:

“Nguvu haiwezi kuwa haki, haki ni lazima ibaki kuwa haki. Hakuna nchi moja inayoweza kuinyanyasa familia yote ya binadamu. Huenda kila mmoja wetu ni dhaifu peke yake, lakini hisia za ukandamizaji na dhuluma zitatufanya tuungane na kuwa nguvu itakayoshinda dhuluma hii.”

Mbali na Subianto, viongozi wengine ambao wamehutubia mkutano, wakiwamo Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil, Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, na Katibu Mkuu wa UN, António Guterres, wote wamezungumzia umuhimu wa kuanzishwa taifa huru la Palestina.

Nchi nyingi za Ulaya, zikiwamo Uingereza na Ufaransa, zimetangaza kutambua taifa huru la Palestina. Pia, ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zipo nchi 11, na nyingine zaidi ya 150 ndani ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambazo zimetambua taifa la Palestina.

Hatua hiyo haijamtisha Trump, ambaye kwenye hotuba yake amesema hana muda wa kusikiliza kinachoelezwa na mataifa hayo, lakini akiendelea kushinikiza Hamas kuwaachia mateka waliobaki wa Israel. Trump katika hotuba yake alisema nguvu za dunia zinapaswa kuhakikisha mateka wa Israel walioko Gaza wanarejeshwa.

“Kama ilivyo kuwahimiza kuendelea kwa mzozo, baadhi ya watu katika taasisi hii wanatafuta kutambua taifa la Palestina peke yao. Zawadi hizo zitakuwa kubwa kwa magaidi wa Hamas kutokana na uharibifu wao,” alisema Trump.

Kauli ya Trump ilikuwa majibu ya moja kwa moja kwa uamuzi wa nchi kadhaa za Ulaya kutangaza kutambua taifa la Palestina. Kutambua taifa la Palestina, Trump alisema, “itakuwa zawadi kwa matendo haya ya kikatili, yakiwemo ya Oktoba 7, 2024.”

Trump alipendekeza njia mbadala ya kidiplomasia:

“Badala ya kukubali madai ya fidia ya Hamas, wale wanaotaka amani wanapaswa kuungana na ujumbe mmoja: Waachilieni mateka sasa, waachilieni tu mateka.

 “Tunalazimika kusitisha vita huko Gaza mara moja. Tunalazimika kuvimaliza… Tunalazimika kuanza mazungumzo mara moja. Lazima tujadiliane kwa ajili ya amani. Tunalazimika kuwarudisha mateka.”

Alichosema Katibu Mkuu wa UN

Kauli ya Trump ilikuwa tofauti na hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliyesema suluhisho ni kuwa na mataifa mawili na kwamba utawala wa taifa la Wapalestina “ni haki, si zawadi.”

Guterres, kwenye hotuba yake, ametaja hali ya Gaza kuwa “isiyovumilika” na kusema kwamba suluhisho la mataifa mawili ndilo “njia pekee ya kutoka kwenye jinamizi hili.”

Kwa mujibu wa Guterres, japokuwa anakaribisha maamuzi ya mataifa mbalimbali ya kutambua suluhisho la mataifa mawili, pia amesisitiza kuwa “hakuna kinachoweza kuhalalisha mashambulizi ya kigaidi ya kutisha ya Oktoba 7, 2024, yaliyofanywa na Hamas au kitendo cha kuchukua mateka. Na hakuna kinachoweza kuhalalisha adhabu ya pamoja dhidi ya watu wa Palestina,” ameongeza.

Akijibu ukosoaji uliotolewa, amesema kuwa kuanzishwa kwa taifa la Palestina “ni haki, si zawadi,” na kwamba pasipo hilo, hakutakuwa na “amani” katika eneo hilo.

“Lazima tujitoe upya katika kutekeleza suluhisho la mataifa mawili kabla ya kuchelewa. Suluhisho ambalo linahusisha mataifa mawili huru, yaliyoungana kijiografia, ya kidemokrasia, yanayoweza kuendelea na yenye mamlaka kamili, yanayotambuliwa kwa pamoja na kuingizwa kikamilifu katika jumuiya ya kimataifa,” amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Kufuatia kauli hizo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, naye ametoa kauli kuwa wale wanaotambua taifa la Palestina “wanatoa zawadi kubwa kwa ugaidi.”

Rais wa Mamlaka ya Palestina

Hata hivyo, Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, akizungumzia kutambuliwa taifa la Palestina amesema kuwa Hamas haipaswi kuwa na “nafasi yoyote” katika kuiongoza Gaza katika siku za usoni na akaitaka kundi hilo la wanamgambo kukabidhi silaha zake.

“Hamas na makundi mengine lazima yakabidhi silaha zao kwa Mamlaka ya Palestina,” Abbas amesema kupitia video katika mkutano wa kilele kuhusu suluhisho la mataifa mawili katika Umoja wa Mataifa, ambapo Ufaransa ilitangaza kutambua taifa la Palestina.

“Kile tunachokitaka ni taifa moja lililoungana lisilo na silaha, taifa lenye sheria moja na vikosi vya usalama halali,” amesema.

Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, naye ametetea utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili kwa ajili ya amani Mashariki ya Kati, taifa la Palestina na taifa la Israel.

“Kinachotokea Gaza si kuangamiza tu watu wa Palestina, bali ni jaribio la kuharibu ndoto yao ya kuwa taifa. Wote Israel na Palestina wana haki ya kuwepo,” amesema.

Kulingana na Serikali ya Brazil, amani, usalama, na utulivu Mashariki ya Kati yanahitaji utekelezaji wa taifa la Palestina huru na lenye uwezo, linaloishi pamoja na taifa la Israel, ndani ya mipaka ya mwaka 1967, ikijumuisha Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, na Jerusalemu Mashariki kama mji mkuu wake.

Katika hotuba yake, pia amesisitiza kwamba suala la Palestina lilianza miaka 78 iliyopita, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokubali Mpango wa Kugawanya, ulioleta matumaini ya mataifa mawili. Hata hivyo, taifa moja tu ndilo lililotokea: Israel.

“Mzozo kati ya Israel na Palestina ni ishara kuu ya vikwazo vinavyokumba mfumo wa ushirikiano wa mataifa mengi. Unaonesha jinsi udikteta wa haki ya kuweka ‘veto’ unavyoharibu maana halisi ya Umoja wa Mataifa, ambayo ni kuzuia ukatili kama ule uliosababisha kuanzishwa kwake urudiwe,” amesema.

Lula pia amesema kwamba Brazil inalaani vitendo vilivyofanywa na Hamas.

Rais Prabowo Subianto, akihutubia mkutano huo, amesema Indonesia inaunga mkono suluhisho la mataifa mawili kama njia ya kukabiliana na mgogoro huko Gaza.

“Lazima tuwe na Palestina huru, lakini pia lazima tukubali na kuhakikishia usalama wa Israel. Ni katika hapo tu ndipo tunaweza kupata amani halisi, amani bila chuki, amani bila kusimama na mashaka. Suluhisho pekee ni suluhisho la mataifa mawili.

“Wenye hatia hawana utajiri wa sauti, wasiokuwa na hatia wanalia msaada, wakiwa na hamu ya kuokolewa. Nani atawasaidia? Nani atawalinda wasiokuwa na hatia? Nani atasimama kwa wazee na wanawake? Wakati tunakaa hapa, mamilioni bado wanakabiliwa na hatari,” amesema.

Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, amewahimiza viongozi wote wa dunia kusimama imara kwa niaba ya Wapalestina waliozidishwa mateso leo.

“Hapa, kwa moyo mkunjufu, nawahimiza wakuu wote wa dola na serikali. Leo ni siku yake. Leo ni siku ya kusimama kwa Wapalestina waliozidishwa mateso kwa niaba ya ubinadamu. Wakati watu wenu wanapochochea dhuluma huko Gaza, kuwa na ujasiri wa kuifuata hatua.”

Rais huyo wa Uturuki aliingia kwenye mkutano huo akiwa na picha mbalimbali zikiwaonesha watoto wanaotaabika kwa vita huko Gaza, wengine wakiwa hawana baadhi ya viungo na wengine wakidhoofika kwa njaa.

Akiinua picha ya mtoto aliye karibu kufa kwa njaa, Erdoğan ameuliza:“Ni dhamiri gani inaweza kustahimili? Ni dhamiri gani inaweza kubaki kimya juu ya hili? Je, kuna amani duniani ambapo watoto wanafariki kwa njaa au kukosa dawa?”