VIDEO: Sura mpya sakata la uvamizi nyumba ya mjane

Dar es Salaam. Wanasheria wa pande mbili katika mvutano wa umiliki wa nyumba iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam, wamezungumzia undani wa mgogoro huo uliosababisha mali za mjane, Alice Haule na wapangaji wake kutolewa nje kwa nguvu.

Alice aliondolewa kwenye nyumba jana Septemba 23, 2025, huku waliohusika katika tukio hilo wakitumia nguvu, wakihusika mabaunsa waliowabeba juujuu mjane huyo na binti yake.

Katika mgogoro huo, inadaiwa Alice ni mvamizi wa nyumba, ambayo yeye anasema waliinunua pamoja na mume wake, Justice Rugaibula (sasa marehemu).

Inadaiwa nyumba hiyo iliuzwa kwa Mohamed Mustapha Yusufali, kwa Sh150 milioni mwaka 2010 kutokana na mkopo uliokopwa na Rugaibula kutoka kwa Yusufali.

Hata hivyo, Alice katika mahojiano na Mwananchi akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jana usiku, Septemba 23, 2025 alikokwenda kwa matibabu akitokea Kituo cha Polisi Oysterbay alieleza taarifa alizonazo ni kuwa, kulikuwa na deni la kiasi hicho cha fedha ambazo mume wake alikopa kutoka kwa Yusufali na siyo kumuuzia nyumba kama inavyodaiwa.



RC Chalamila atoa maelekezo sakata la uvamizi nyumba ya mjane

Wakizungumzia mgogoro huo wanasheria Hajra Mungula anayemwakilisha Yusufali na Mwesigwa Muhingo anayemwakilisha Alice, wameeleza ilivyokuwa hadi kufikia hatua iliyopo sasa.

Kwa nyakati tofauti leo Septemba 24, 2025 wanasheria hao wamesema Alice na Yusufali wamewahi kusuluhishwa nje ya Mahakama miaka mitatu iliyopita lakini ikashindikana.

“Tumewahi kuzungumza nje ya Mahakama mwaka juzi (2023) lakini hatukupata muafaka,” amesema Mwesigwa.

Amesema Yusufali amekuwa akitaka nyumba ya Alice, akidai ni yake, jambo lililosababisha mteja wake akafungue kesi Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Ijumaa iliyopita (Septemba 19).

“Ilipofika Jumatatu (Septemba 22) ikaonekana ipo rejected (imekataliwa), niliambiwa sikuandika namba ya simu ya Mohamed ambayo sikuwa naifahamu, nilirekebisha na leo (Jumatano, Septemba 24) imekuwa approved (imekubaliwa). Tunasubiri tupewe control namba ili tulipie tupewe namba ya kesi,” amesema.

Mwesigwa amesema katika maombi yao, miongoni mwa wanayoomba ni Mahakama itamke nyumba ambayo Yusufali anasema aliuziwa ni ya marehemu Justice Rugaibula. Anadai makubaliano ya mauziano ni ya kughushi na familia ya marehemu haikuwa ikiyafahamu.

Mungula kwa upande wake ameeleza mgogoro ni wa muda mrefu na uliwahi kusuluhishwa nje ya Mahakama pasipo mwafaka kufikiwa.

“Yusufali alisema tangu 2011 aliwekeza pesa yake ambayo imesimama muda wote bila kuzalisha. Alitaka wam- compensate (wamfidie) na Alice aangalie jinsi gani atam- compensate,” amedai na kuongeza:

“Alice alikuja na ofa ndogo, Yusufali akaja na ofa kubwa, ni kama mmoja aje na ofa ya milioni tatu, mwingine aje na ofa ya milioni 20, hakukuwa na muafaka, huyu alisema hivi na yule akasema vile.”

Amedai mvutano uliibuka upya baada ya Alice kupangisha nyumba hiyo, tofauti na awali alipokuwa akiishi mwenyewe.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Alice, ana wapangaji ambao ni Wachina wanaoishi nyumba tofauti na anayoishi yeye. Mali za wapangaji hao zilitolewa nje jana Septemba 23. Wapangaji wanaishi nyumba ya mbele naye na familia yao iko nyuma.

Mungula anadai katika mvutano huo, Yusufali na Alice wameshindwa kufikia mwafaka hadi pale mteja wake alipoamua kufuata utaratibu uliotumika jana, Septemba 23.

Akizungumzia tukio hilo akiwa kwenye nyumba yenye mgogoro leo Septemba 24, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi amesema watafuatilia kumbukumbu zote za uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria.

“Shauri lao ni la tangu 2011, tutajitahidi kufikia kumbukumbu zote za uchunguzi na kuchukua hatua,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyefika katika nyumba hilo amesema katika mvutano huo kuna mambo makubwa mawili, kwanza ni kesi anayoisema Alice ipo au haipo na anamiliki nyumba hiyo au hapana.

“Jambo la pili ni njia iliyotumika kumtolea vitu nje ni ya kudhalilisha,” amesema.

Chalamila amesema Alice anakiri mwaka 2011 aliona mume wake anataka kuuza au kuweka rehani nyumba yake.

Amesema mwaka 2012 alishtuka kwamba inawezekana mume wake anataka kuuza nyumba na kwenda Wizara ya Ardhi kuweka zuio, tayari hati ya nyumba ilishakuwa transferred (imehamishwa umiliki), hivyo amesema kuna haja ya kuangalia namna gani suala hilo litamalizwa na sheria ichukue mkondo wake bila kumuonea wala kumpendelea yeyote.

Amezitaka pande zote mbili kufika ofisini kwake Ijumaa Septemba 26 ili kuzungumzia hilo.

“Kama shida ilikuwa hela, angesema marehemu mume wangu hakumlipa mimi ningejua namlipaje, lakini si kudai nyumba ni yake,” ni kauli ya Alice alipozungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jana Septemba 23.

“Sijui walikopeshana vipi, lakini ninavyosikia mume wangu na huyu mtu Yusufali walikuwa wakifahamia tangu mwaka 2010 na kukopeshana Sh150 milioni,” amesema.

Alice amesema mwaka 2012 Yusufali alifanya jaribio la kumuondoa kwenye nyumba kama ilivyofanyika jana, wakati huo mume wake alikuwa hai ikashindikana.

“Mume wangu alisafiri kwenda Afrika Kusini, mimi nikiwa kwenye shughuli zangu Kariakoo, nikapigiwa simu nyumba yangu imevamiwa, bahati nzuri polisi waliwahi wakanisaidia kuzuia,” amesema.

Amedai baada ya tukio hilo alikwenda Wizara ya Ardhi kuweka zuio akidai Yusufali alikuwa na hati ya kughushi.

“Wizara ilitaka mume wangu akirudi kutoka Afrika Kusini wamalizane. Niliona document (nyaraka) mume wangu akieleza hakumuuzia nyumba, alimkopa pesa. Nikasikia baadaye walilipana na mume wangu akataka arudishe hati ya nyumba,” amedai.

Amesema suala hilo lilikwenda likawa kimya, hivyo akajua tayari wamemalizana na limepita, kwa kuwa, Yusufuali aliondoka nchini.

“Mwaka 2022 mume wangu alifariki dunia, ajabu miezi ya hivi karibuni nikaanza kupata vitisho kutoka kwa Yusufuali akiniita mvamizi kwenye nyumba yangu,” amedai.

Akizungumzia tukio la vitu kutolewa nje amesema Ijumaa iliyopita, Septemba 19 alifungua kesi Mahakama ya Ardhi akidai hati ya nyumba yake.

Amedai pia aliwasilisha taarifa polisi kuhusu kosa la jinai la kughushi hati hiyo, lakini wakati wakiendelea na taratibu nyingine za kisheria ndipo watu wakavamia nyumba hiyo na kutoa vitu nje, wakishinikiza yeye ni mvamizi.

“Nilipigiwa simu na Serikali ya mtaa wakaniambia wamepata barua inatakiwa vitu vyangu vitolewe nje. Wakati watu hao wamefika nyumbani na kuanza kutoa vitu nilikuwa nimekwenda polisi kuomba msaada,” amesema na kuongeza:

“Nikatoka polisi na bodaboda nikakuta wamevunja geti, ndani kuna mabaunsa kama 18, nikaanza kupiga yowe, wakaanza kunipiga wakitoa vitu kwenye nyumba ya wapangaji wangu (Wachina) ipo mbele na kwangu ni nyuma, zote akidai ni zake.”

Akigumia kwa maumivu, amesema watu hao walimpiga na kumbeba juujuu kumtoa nje, kabla ya kuondoka baada ya waandishi wa habari kufika.

Alice amedai nyumba hiyo waliinunua pamoja na mume wake kwa gharama ya Sh470 milioni.

Amesema wakati mume wake akikopa fedha, yeye hakuhusishwa, akieleza atapambania haki yake hadi mwisho.

Awali, kabla ya kwenye Hospitali ya Mwananyamala, Alice na binti yake alikwenda Kituo cha Polisi Oysterbay.

Kutokana na tukio hilo, Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram ameandika:

“Asante kwa ushirikiano, mama mjane amenitumia sms, nikampigia, nikamsikiliza. Kifupi amesema, mwanasheria anaye, kesi iko Polisi na pia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni anajua jambo hili.”

“Hata hivyo, changamoto zilizotokea ni huko kuvamiwa ghafla bila taarifa na kinyume na utaratibu stahiki wa kisheria ukizingatia kuwa, kesi iko Polisi. Hivyo, msaada wa haraka anaohitaji ni ulinzi wake na mali zake na dhidi ya hayo matishio anayopata.”

Kuhusu hatua alizochukua amesema amewasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na RPC Kinondoni na kuomba, wafanye hatua stahiki ili mama mjane kwanza, awe salama na utulivu kisha, hayo ya kisheria yaendelee kwa mujibu wa sheria ambapo, viongozi wote hao wamepokea kwa hatua stahiki.

“Aidha, saa 9:11 jioni nimeongea tena na mama mjane, ameniambia ni kweli polisi walienda na wale waliokuwa wanamfanyia vurugu walitawanyika na sasa hali iko kwenye utulivu,” ameandika.

Dk Gwajima ametoa wito kwa wanaodai kununua nyumba ya mjane akisema:

“Ndugu, hata kama mnadaiana, tafadhali fuateni taratibu halali za kisheria kupitia kwa mwanasheria wa mjane huyu. Hata katika mapito ya kisheria, tafadhali kumbukeni kuwa na subira na utu uwe kwanza na hapo ndiyo kila mmoja atapata haki yake na Mwenyezi Mungu atapendezwa nanyi nyote na kuwabariki wote. Amina.”

Amesema: “Tuendelee kushirikiana kuzuia changamoto za kijamii na kuibua zinapotokea na kuzipatia mwongozo stahiki kwa wakati.”