‘Waandishi wa habari msiwe maofisa uhusiano wa wagombea’

Shinyanga. Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Nyanda Shuli, amewataka waandishi wa habari kuepuka kuwa maofisa mahusiano wa wagombea, na badala yake kutumia kalamu zao kwa uadilifu katika kutoa taarifa sahihi kwa umma.

Amesema ni muhimu vyombo vya habari vikazingatia maadili ya taaluma yao ili kusaidia kulinda amani na mshikamano wa jamii hususan katika kipindi cha uchaguzi.

Akizungumza leo, Septemba 24, 2025, katika mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Tarura, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Kamishna huyo amewasihi waandishi kuwa kioo cha jamii kwa kuripoti habari kwa haki, usawa na uadilifu.

“Hususan katika kipindi cha uchaguzi, tendeeni haki kalamu zenu kwa kufuata taaluma ya uandishi wa habari kuepuka kuwachanganya wananchi na kusababisha uvunjifu wa amani na kuharibu sifa ya mwandishi kwa umma, kuna baadhi ya waandishi hufanya kazi kulingana na mgombea fulani anachotaka hasa wakati huu wa kampeni kitu ambacho si cha kitaaluma,” amesema Shuli.

New Content Item (1)


New Content Item (1)

Naye Ofisa Mchunguzi Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Brighton Mwiga, amewakumbusha waandishi wa habari kuhusu wajibu wao wa kuripoti taarifa kwa umma kwa njia inayochangia kulinda amani na utulivu wa wananchi.

“Waandishi wa habari tunafanya kuwakumbusha tu wajibu wenu kwa sababu hakuna kitu kigeni, kila kitu kinajulika hasa wakati wa uchaguzi tunawakumbusheni kuwa hakuna mwandishi anayeruhusiwa kuingia na kumrekodi au kumpiga picha mpiga kura akiweka tiki hii ni uvunjifu wa sheria za uchaguzi,” amesema Mwiga.

Aidha, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru, kwa niaba ya waandishi wenzake, ameishukuru tume hiyo kwa kutoa mafunzo hayo muhimu na kuwakumbusha waandishi kuhusu wajibu wao, hususan katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi na kuelekea siku ya upigaji kura.

Mafunzo hayo yametolewa kwa waandishi 20 wawakilishi wa baadhi vyombo vya habari mkoani Shinyanga ikiwemo Mwananchi Communication Limited (MCL), huku Mwiga akiwataka waandishi wa vyombo vingine kuiga mfano wa MCL kutokana na stori iliyotoka Septemba 24, 2025 ukurasa wa mbele ‘Ni kilio cha ukata’ kwa kufuatilia kujua ni kwa nini vyama pinzani havifanyi kampeni.