Wanafunzi msingi wapewa elimu ya usalama barabarani

Dodoma. Wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Mnadani iliyopo Jijini Dodoma wamepewa elimu ya usalama barabarani ili kujilinda na ajali wakati wa kwenda shuleni na kurudi nyumbani.

‎‎Aidha, wanafunzi hao wamefundishwa  alama muhimu za kuvuka barabara kwa usalama ili wasigongwe na magari kutokana na shule yao kupakana na barabara kuu ya kwenda Wilayani Kondoa.

‎‎Wakizungumza wakati wakipokea mafunzo hayo ya usalama barabarani kutoka kampuni ya TotalEnegies leo Jumatano Septemba 24, 2025 jijini Dodoma wanafunzi wanaosoma shule hiyo wamesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo huwa zinatokea mara kwa mara.

‎‎Rebecca Lambai amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua alama za vivuko vilivyoko barabarani, hivyo watavitumia kuvuka barabara kwa usalama na kuepusha ajali.

‎‎”Tumeambiwa tusivuke barabara kwa kukimbia kwani tunaweza kukutana na gari ambalo lina mwendo mkali na kusababisha ajali, pia tumeambiwa tutembee upande wa kulia wa barabara ili tuweze kuona magari yaliyopo mbele na yanayokuja nyuma,” amesema Lambai.

‎‎Naye Johnson Jeremia amesema wamefundishwa alama za vivuko barabarani ambavyo wanatakiwa kuvitumia wakati wa kuvuka barabara ili kuepusha ajali.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Mnadani iliyopo Jijini Dodoma wakimsikiliza Mwalimu wa usalama barabarani (hayupo pichani) leo Septemba 24, 2025. Picha na Rachel Chibwete



‎‎Ametaja alama hizo kuwa ni alama ya watembea kwa miguu ya pundamilia, taa za kuongozea magari, matuta ya barabarani na trafiki na kwamba kabla ya kuvuka barabara wanatakiwa kuchukua tahadhari za kuangalia pande zote ili kuhakikisha hakuna chombo cha moto kilicho karibu ndipo wavuke.

‎‎ Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Jesi Jankeni amesema elimu ya usalama barabarani imekuja kwa wakati muafaka kwa sababu shule hiyo ipo karibu na barabara kuu ya kwenda Wilayani Kondoa hivyo itasaidia kupunguza matukio ya ajali kwa wanafunzi.

‎Amesema pamoja na kutolewa kwa elimu hiyo, lakini bado shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya kukosa uzio na hivyo kusababisha baadhi ya madereva kuingia shuleni hapo na kuhatarisha maisha ya wanafunzi.

‎‎Mwalimu huyo awameowamba wadau hao kuwajengea uzio ili kuzuia madereva wa bodaboda na bajaji kuukatisha katikati ya shule na kuhatarisha maisha ya wanafunzi wa shule hiyo.

‎‎ Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano kutoka TotalEnegies, Getrude Mpangile amesema mradi huo unatekelezwa kwenye shule saba nchini za msingi na sekondari lengo likiwa ni kupunguza ajali kwa wanafunzi.

‎‎Amesema shule zinazotekeleza mradi huo ni za umma zilizopo karibu na barabara kwani wanafunzi wengi wanaosoma shule hizo ndiyo huwa wanatembea kwa miguu kuvuka barabara pindi wanapotoma shule na kurudi nyumbani.

‎‎”Mpaka sasa tuna shule saba ambazo zinatekeleza mradi huu wa usalama barabarani kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na kwa mara ya kwanza tumekuja hapa Dodoma kutekeleza mradi huu kwa Shule ya Msingi Mnadani,” amesema Mpangile.

‎‎Amesema mafanikio ya elimu hiyo ni makubwa kwani shule, wanafunzi na jamii wameitikia kwa kiasi kikubwa kwani elimu inayotolewa imesaidia kupunguza ajali za barabarani kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule ambazo ni lazima wavuke barabara.

‎‎”Tumeamua kuwekeza elimu hii kwa watoto kwa sababu mtoto ukimfundisha kitu habaki nacho peke yake bali anawaelimisha wengine na hili tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu tunashirikiana na kikosi cha ulama barabarani ambao huwa wanatoa elimu kwa vitendo,” amesema Mpangile.