Mbeya. Wananchi katika mitaa ya Soweto, Block Q na Kagera jijini Mbeya wamesema wanaanza kuhofia afya zao ikiwamo kupata mlipuko wa magonjwa kutokana na maji wanayotumia, kufuatia huduma hiyo kukosekana kwa takribani wiki mbili.
Hata hivyo Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira jijini humo (Mbeya Uwsa) imesema inafuatilia changamoto huyo kwa kufika maeneo hayo ili kujiridhisha na kufanyia kazi haraka.
Mwananchi Digital imefika baadhi ya maeneo hayo na kushuhudia wananchi wakipata huduma ya maji katika visima na Mto Kagera, huku wengine wakifua nguo katika eneo hilo.
Wakizungumza leo Septemba 24,2025 baadhi ya wananchi hao, wamesema huduma ya maji imekuwa changamoto hali inayowafanya kutumia maji yasiyo na ubora.
Abison Mwanike amesema ni takriban mwezi mmoja hawana huduma hiyo, hali inayowapa hofu kuhusu usalama wa afya zao, kwa sababu maji wanayotumia kwa sasa kutokuwa salama akiomba Serikali kuwahurumia.
“Kero hii ni kubwa sana katika maeneo haya, tunatumia mifereji kupata maji ambapo kiuhalisia si sahihi, tuna hofu hata magonjwa ya mlipuko kutukabili, tunaomba watusaidie, hatuna maji kwa mwezi sasa,”amesema Mwanike.
Naye Rehema Charles amesema kwa baadhi ya maeneo ya mitaa hiyo, huduma hiyo hupatikana nyakati za usiku lakini kwa sasa hali si shwari.
Amesema ni muda mrefu hawajapata maji safi, akieleza kuwa kilio chao ni kuona wenye mamlaka husika wanawasaidia ili kuondokana na kadhia wanazopitia.
“Tunatumia haya maji kwa kuchemsha, tunaamka mapema sana kuwahi pia foleni, kama kuna sehemu yanatoka ni usiku sana, tunaomba watusaidie,” amesema Rehema.
Naye Seleman Mkina amesema pamoja na kukata kwa huduma hiyo, bado wanapokea bili za gharama kubwa tofauti na matarajio akiomba wenye mamlaka kulitazama upya ili kuwapunguzia mzigo.
“Kipindi maji yanatoka muda mwingine bili inakuja ya kawaida, lakini kwa sasa ambapo maji hayatoki tunapata bili kubwa hadi tunashangaa, hebu watusaidie wenye mamlaka tulipe tunachotumia,” amesema Mkina.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi digital Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini humo (Mbeya Uwsa), Neema Stanton amesema bado hawajapata taarifa hizo akiahidi kufuatilia na kumaliza kero hiyo.
“Naomba nifuatilie hizo taarifa kwakuwa wao wameongea ila lazima nijiridhishe aidha kwa kufika maeneo hayo ili nijue changamoto ilipo na hapo nitakuwa na cha kuzungumza,” amesema Neema.