Dar es Salaam. Kampuni na taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika maonesho ya biashara ya ujenzi, Afrika Mashariki yajulikanayo kama Buildexpo Tanzania 2025, zimetakiwa kuwekeza nchini kwa kuanzisha viwanda badala ya kuishia kushiriki maonyesho na kuzalisha bidhaa katika mataifa mengine.
Wito huo umetolewa leo Jumatano Septemba 24, 2025 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janeth Lekashingo wakati akifungua maonyesho hayo yanayofanyika kwa siku tatu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Lekashingo amesema upatikanaji wa vifaa na teknolojia hapa nchini utasaidia kuokoa muda na gharama, hususan kwa kupunguza uagizaji kutoka nje ambao mara nyingi hutumia fedha za kigeni.
“Tukiwa na teknolojia za kujenga na kukarabati zinazopatikana humu nchini, itapunguza muda wa kusubiri vifaa kutoka nje, lakini kubwa zaidi ni kupunguza gharama kwa sababu vingi vinaagizwa kwa dola za Marekani. Migodi tunayo, Watanzania tupo tayari kushiriki, ndiyo maana tumeanzisha hadi ukanda maalum wa Buzwagi,” amesema.
Amesema sekta ya madini mpaka sasa imetoa ajira kwa zaidi ya watu milioni 1.2 ikiwa ni pamoja na ajira za moja kwa moja na zile za mikataba.
Akizungumzia umuhimu wa maonyesho hayo, Lekashingo amesema yanasaidia kuongeza uelewa, kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu maendeleo ya teknolojia katika sekta ya madini na ujenzi kwa ujumla.
“Naomba Watanzania waje kwa wingi kuyatembelea maonesho haya. Niamini hawatatoka bure, watapata maarifa mapya na fursa nyingi,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Biashara ya Nje (TanTrade), Latifa Khamis akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah, amesema Serikali imetengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji wa viwanda, ikiwemo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uzalishaji.
Amebainisha kuwa uzalishaji wa bidhaa hizo nchini, utachangia kukuza uchumi na kutekeleza kwa vitendo kampeni ya Made in Tanzania.
Awali, Mratibu wa maonyesho hayo, Danken Njage amesema lengo kuu la Buildexpo Tanzania ambayo mwaka huu yanafanyika kwa mara ya 26, ni kuunganisha bidhaa, teknolojia na suluhisho bunifu katika sekta ya ujenzi na miundombinu.
Njage amesema washiriki na wageni wanapata fursa ya kukutana na viongozi wa sekta, wasanifu majengo, wahandisi, makandarasi, wazalishaji na wasambazaji huku maelfu ya bidhaa na huduma zikioneshwa wazi.
Amesema zaidi ya kampuni 200 kutoka nchi 30 ikiwamo China, India, Afrika Kusini, Ujerumani, Kenya, Uturuki, Korea Kusini, Italia na Hispania, zimeshiriki katika maonyesho hayo.
“Wingi wa washiriki mwaka huu umechochewa na ukuaji wa uchumi wa Tanzania, unaotokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama reli ya kisasa ya SGR, bandari ya Bagamoyo, mradi wa gesi asilia ya kimiminika (LNG) na bomba la mafuta ghafi la EACOP. Miradi hii inafungua fursa mpya za uwekezaji katika sekta za ujenzi, nishati na mali isiyohamishika,” amesema.