Watatu walioshtakiwa kumuua bodaboda, wahukumiwa kunyongwa

Arusha. Watuhumiwa watatu kati ya wanne walioshtakiwa kwa mauaji ya dereva bodaboda, Shaban Mwalile, wamehukumiwa adhabu ya  kunyongwa hadi kufa.

Mwenzao mmoja aliyekuwa ameshtakiwa nao, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kukiri kosa la kusaidia kuficha taarifa za mauaji hayo, chini ya kifungu cha 213 cha kanuni ya adhabu.

Washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa ni Denis Swai, Musa Bushiri, na Alhaji Likwaya huku aliyekuwa mshtakiwa wa pili, Athumani Mpango, akihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.

Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 19,2025 na Jaji Stephen Magoiga, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Morogoro.

Hukumu hiyo ambayo nakala yake imepakiwa katika mtandao wa mahakama, imeeleza baada ya Mahakama kupitia ushahidi wa pande zote mbili imejiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri, ulithibitisha bila shaka kuwa washtakiwa hao watatu walihusika na mauaji hayo.

Watuhumiwa wote wanne walikabiliwa na shtaka la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, kwa tukio lililotokea Septemba 5, 2024, katika Kambi ya Uvuvi ya Senga, eneo la Ipatilo, Kata ya Minepa, ndani ya Pori la Akiba la Kilombero, mkoani Morogoro.

Ilielezwa kuwa Shaban, ambaye alikuwa dereva bodaboda, alikodiwa na Denis na Athumani kwa ajili ya kwenda kutafuta mashamba katika eneo la Ipatilo.

Walipofika eneo hilo, wakiwa na washtakiwa wa tatu na nne, walimuua Shaban, wakamvua nguo zake, kisha kuiba pikipiki yake.

Uchunguzi ulianza baada ya taarifa za kupotea kwa Shaban kusambaa mjini Ifakara, ambapo Jeshi la Polisi lilianza kufuatilia simu ya mwisho iliyopigwa kwa marehemu, na kugundua kuwa simu hiyo ilikuwa ya mke wa Athumani, ambaye aliwezesha kukamatwa Athumani na wenzake.

Denis na Athumani walipohojiwa, waliongoza polisi hadi sehemu walipokuwa wameacha mwili wa marehemu.

Upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 16 akiwemo Musa Abdurahman, Ofisa wa kliniki mwandamizi wa Kituo cha Afya Kibaoni, aliyeieleza Mahakama kuwa alikuta mabaki ya mwili wa mtu katika eneo la Ipatilo na alithibitisha kuwa yalikuwa mifupa ya binadamu.

Alisema kuwa mifupa pekee haikuweza kutoa ushahidi wa chanzo cha kifo.

Shahidi mwingine, Tambwe Ismail ambaye ni dereva bodaboda alieleza jinsi alivyowaona washukiwa wakiwa na marehemu, na alithibitisha kuwa aliwatambua Denis na Athumani katika gwaride la utambulisho.

Shahidi wa nne ambaye pia alikuwa dereva bodaboda, Said Hamis, alieleza kuwa aliiona pikipiki ya marehemu ikiwa na washukiwa, na alitambua baadhi ya vitu alivyovihifadhi Shaban, kama kamba nyekundu, katika eneo la tukio.

Shahidi wa 16,Sajenti Abdallah, aliyeandika maelezo ya onyo ya  Musa, alieleza kuwa mshtakiwa huyo alikiri shtaka hilo na kuwa alishirikiana na wenzake.

Katika utetezi wao, washtakiwa walikanusha kuhusika na mauaji.
Denis alidai kuwa alilazimishwa kutoa maelezo ya onyo na alikana kuwaongoza polisi hadi eneo la tukio na kukana hakupokea fedha za mauzo ya pikipiki ya marehemu.

Athumani alikiri kushirikiana na Denis kupanga wizi wa pikipiki, lakini alikataa kuwa na nia ya kumuua Shaban. 

Mshtakiwa huyo aliiambia Mahakama kuwa alifahamiana na mshtakiwa wa tatu na wa nne kupitia Denis (mshtakiwa wa kwanza), ambapo aliwasikia katika mazungumzo yao wakipanga kuiba pikipiki ila alielewa kuwa wanapanga kuiba tu na siyo kufanya mauaji.

Alisema Septemba 5,2024 akiwa na wenzake katika eneo la tukio, Denis alimshika Shaban (marehemu kwa sasa) shingoni, Hamad akamshika miguu na Musa akampiga kabla ya kumnyonga shingo hadi akafariki.

Aliieleza Mahakama kuwa alitishiwa na wenzake waliomtaka kutosema kuhusu tukio hilo ambapo walipomaliza walimvua marehemu nguo, wakachukua fedha, simu na pikipiki kisha wakachukua mwili wake na kuuburuza hadi porini.

Kwa upande wake Musa alikana kuhusika na mauaji, akidai kuwa hakushiriki katika tukio hilo na alikana maelezo yake ya onyo.
Alhaji alikana kumfahamu marehemu na alisema kuwa alilazimishwa kusaini maelezo ya onyo na kuwa alimfahamu mshtakiwa mmoja tu (Musa) kwani walisoma pamoja.

Jaji Magoiga amesema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi ni wajibu wa Mahakama kuchambua ushahidi ili kubaini iwapo kesi dhidi ya washtakiwa imethibitishwa pasipo shaka yoyote.

Jaji amesema mambo muhimu ya kuzingatia ni kama kweli Shaban alifariki dunia, kifo kilikuwa cha kawaida au laa, kama washtakiwa ndio walihusika na kama mauaji hayo yalikuwa ya kukusudia au laa.

Amesema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, hakuna ubishani kuwa Shaban alifariki dunia na mabaki ya mwili wake kukutwa porini na kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida.

Jaji amesema sheria inawalazimu upande wa mashtaka chini ya kifungu cha 3 (2)(a) cha Sheria ya Ushahidi, kuthibitisha kesi yake bila shaka yoyote na kwamba kila mshtakiwa alishiriki katika mauaji ya Shaban.

Baada ya uchambuzi amesema kuhusu nani aliyesababisha mauaji, hakuna shahidi wa mashtaka hata mmoja aliyethibitisha kuwaona washtakiwa katika kesi hiyo wakimuua Shaban, isipokuwa mshtakiwa wa pili ambaye aliona kilichotokea.

Amesema katika maelezo ya onyo na maelezo ya ziada, Athuman (mshtakiwa wa pili) ,alieleza mpango mzima ulikuwa kupora pikipiki lakini mshtakiwa wa tatu na nne walipoona Shaban anawafahamu, waliamua kumuua.

Jaji huyo ameongeza kuwa utetezi wa washtakiwa wengine ulikuwa wa jumla mno na hivyo haukutikisa ushahidi wa jinsi walivyopanga, kufadhili na kutekeleza mauaji ya Shaban.

“Kuhusu mshtakiwa wa kwanza, tatu na nne na yote yaliyozingatiwa ni maoni yangu kwamba walifanya juhudi za pamoja kumuua mshtakiwa kama walivyoshtakiwa. Mshtakiwa wa pili nimepitia ushahidi hakuna shahidi aliyethibitisha kuwa alikuwa na mpango wa kumuua Shaban na hakuwa na nia mbaya ya kushiriki mauaji hayo,”amesema.

Jaji aliwahukumu Denis, Musa, na Alhaji adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kuwakuta na hatia ya mauaji hayo,  huku Athumani akihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.