KINARA wa upachikaji mabao msimu uliopita ndani ya Ligi Kuu Bara, Charles Ahoua ameendelea alipoishia msimu uliopita akiitesa Fountein Gate baada ya kufunga na kuasisti Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Ahoua msimu uliopita dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa KMC Complex Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0, alifunga bao moja na kutoa pasi mbili zilizozaa mabao kwenye mchezo huo mabao. Mengine yalifungwa na Edwin Balua, Steven Mukwala na Valentino Mashaka.
Leo kiungo huyo aliyetupia mabao 16 msimu uliopita, ameendelea alipoishia akitoa pasi iliyozaa bao dakika ya tano ya mchezo baada ya kuchonga kona iliyounganishwa kwa kichwa na beki Rushine De Reuck.

Licha ya Fountain Gate kuingia kinyonge na kushindwa kuendana na kasi ya mchezo, Elie Mokono hakutaka kuonyesha unyonge akijaribu mara kwa mara kulenga lango la Simba akiwa nje ya 18 na kuisaidia timu hiyo kuambulia kona moja dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Kona ya Fountain Gate haikuwa na madhara langoni mwa Simba kutokana na umakini wa safu ya ulinzi ya timu hiyo licha ya majaribio mengine ya mara kwa mara nje ya 18.
Ahoua alitumia dakika 37 kuifungia Simba bao la pili baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa kiungo mkabaji, Yusufu Kagoma na kukwamisha mpira nyavuni.
Mabao hayo yalidumu hadi dakika ya 45 kipindi cha kwanza huku Fountain Gate ikiambulia kuchonga kona moja pekee hadi mwamuzi alipopuliza kipyenga kuashiria mapumziko.

Kipichi cha pili Simba ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mzamiru Yassin na Kibu Denis nafasi zao zilichukuliwa na Morice Abraham na Alassane Kante, mabadiliko yaliyoongeza burudani kwa mashabiki wachache waliojitokeza kwa Mkapa.
Mchezo ulikuwa unachezwa upande mmoja huku kipa wa Simba, Moussa Camara mara kadhaa akisogea juu kutoa maelekezo kwa wachezaji wenzake.
Dakika ya 57, Jonathan Sowah alishindilia msumari wa tatu akipokea krosi kutoka kwa Elie Mpanzu.

Simba ilifanya mabadiliko tena ikimtoa mfungaji wa bao la kwanza, Rushine De Reuck, nafasi yake ilichukuliwa na Wilson Nangu, pia alitoka Shomari Kapombe akaingia David Kameta na Yusuph Kagoma akampisha Neo Maema.
Licha ya kipindi cha pili Simba kuonesha kiwango kizuri kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi, ilishindwa kutumia nafasi ilizotengezeza kwa kuingia mara kwa mara langoni kwa Fountain Gate na kujikuta ikimaliza mchezo kwa ushindi wa mabao hayo.