Askofu Mkuu Rugambwa anavyokumbukwa Vatican

Dar es Salaam. Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, ameongoza misa ya kumuombea na kumuaga, Askofu Mkuu Novatus Rugambwa, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Vatican, vilevile walikuwapo Askofu Mkuu Msaidizi wa Vatican,  Edigar Pena Para, maaskofu wakuu, maaskofu na mapadri katika misa hiyo iliyoadhimishwa leo Septemba 25, 2025.

Katika mahubiri, Kardinali Parolin amesema: “Tunaadhimisha misa hii kwa ajili ya mazishi ya Askofu Mkuu Novatus Rugambwa ambaye Septemba 16, 2025 aliaga dunia baada ya ugonjwa wa muda mrefu.”


Amesema baada ya miaka mingi ya shughuli zake za kitume: “Bwana alimwomba mchango wa Kanisa, ule wa mateso kuyatoa katika muungano na Kristo kwa ajili ya wokovu wa ndugu. Alikabiliana kwa imani yake na mfano wa upendo katika ugonjwa, kwa kufanya hata katika fursa hii, kujibakidhi kwa mapenzi yake na kwa ujenzi wa watu wa Mungu, hasa wale wote ambao kwa imani walimuuguza na kumfuatilia hadi mwisho wa maisha yake hapa duniani.”

Amesema ameacha ushuhuda unaoweza kusaidia kutafakari juu ya kile ambacho Mtakatifu Paulo aliwaandikia Wakristo wa Roma na leo hii Liturujia inapendekeza kwa umakini na sala kwamba: “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu (Rm 8:18)”


Amesema Askofu Mkuu Rugambwa anajiwakilisha mbele ya Mungu na sadaka kubwa aliyotimiza, ikiwamo ukarimu na upendo.

“Alitoa mfano mzuri, kwa uthabiti wake wa maisha ya huruma, busara yake na wakati huohuo, kwa uthabiti katika kutetea misingi ya haki na heshima ya mtu, ambayo ni muhimu  kwa ajili ya kuishi kwa amani licha ya utofauti, mbali na mipaka ya kitaifa,” amesema.

Kardinali Parolini pia amemkumbuka kwa uadilifu wa maisha aliyokuwa nayo, ya ushuhuda wa mamlaka na uaminifu wa ukweli ambao aliutangaza.

Akizungumzia somo la Injili kuhusu hukumu ya mwisho (Mt 25, 31-46) amesema: “Inakumbusha kile ambacho tutahukumiwa mwishoni mwa mchakato wa maisha hapa duniani, hayatakuwa mafanikio, wala kushindwa, bali upendo ambao tuliutoa kwa kile tulichopokea.”


Licha ya maaskofu, mapadri kutoka sehemu mbalimbali za dunia na hasa alikozaliwa Bukoba, Tanzania na mahali alikofanya kazi, misa pia ilihudhuriwa na waamini na wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali, wakiwamo kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.

Askofu Mkuu Rugambwa alizaliwa Oktoba 8, 1957, katika Jimbo Katoliki la Bukoba, nchini Tanzania. Baada ya masomo na majiundo ya kikasisi, akapewa daraja takatifu ya upadre mikononi mwa hayati Askofu Nestorius Timanywa Julai 6, 1986.

Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican Julai mosi, 1991.

Baada ya kufanya kazi mbalimbali katika balozi za Vatican, Juni 28, 2007 Papa Benedikto wa XVI alimteua kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalumu.

Februari 6, 2010, Papa Benedikto XVI, alimteua kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tome na Principe na kuwekwa wakfu kuwa Askofu Mkuu na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Vatican kwa wakati huo, Machi 18, 2010.


Machi 5, 2015 aliteuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Honduras. Machi 29, 2019, Papa Francisko alimteua kuwa Balozi wa Vatican nchini New Zealand na mwakilishi wa kitume kwenye visiwa vya Bahari ya Pacific.

Machi 30, 2021, Papa Francisko alimwongezea majukumu kwa kumteua kuwa Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Microsia, iliyoko Magharibi mwa Bahari ya Pacific.


Wakati huohuo aliendelea kuwa Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Marshall, Kiribati, Nauru na Tonga. Pia Balozi wa Vatican nchini New Zealand, Fiji, Palau na Mwakilishi wa Kitume kwenye Bahari ya Pacific.

Juni 10, 2025, akiwa mgonjwa Askofu Mkuu Rugambwa alishiriki mkutano wakati Papa Leo XIV, alipokutana na mabalozi wote wa Vatican wanaomwakilisha maeneo yote duniani. Alikuwa akitumia kitimwendo.