Njombe. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewaahidi wananchi wa Makambako ujenzi wa stendi mpya ya mabasi na soko la kisasa ili kuwaondolewa adha ya muda mrefu hususan nyakati za mvua.
Pia, Dk Nchimbi amesema Serikali ya CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inakwenda kusimamia vyema sera ya ulipaji kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili ziwe rafiki kwa wafanyabiashara.
Dk Nchimbi ametoa ahadi hizo Jumatano, Septemba 24, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Uwanja wa Polisi, Makambako, Mkoa wa Njombe.
Ahadi hizo zimetolewa wakati akijibu changamoto zilizowasilishwa kwake na mgombea ubunge wa Makambako, Daniel Chongolo ambaye ametumia fursa hiyo pia kueleza mafanikio ya miaka minne na nusu ya utawala wa Rais Samia.
Mbali na suala hilo la soko na stendi, Chongolo ameelezea umuhimu wa ujenzi wa barabara za Makambako zinazounganisha eneo hilo na mikoa na nchi kadhaa zikiwemo Malawi, Zambia, Congo, Afrika Kusini, Msumbiji na Zimbabwe.
Ni katika mkutano huo Dk Nchimbi amemshukuru Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Njombe, Deo Sanga maarufu Jah People kwa kuonesha mfano wa kukubali matokeo kwa kutoteuliwa kwake.

Katika mbio za ubunge wa Makambako, Jah People aliyekuwa akitetea jimbo hilo, alichuana vikali na Chongolo. Kura za maoni Chongolo alimshinda kwa mbali na Halmashauri Kuu ya CCM ikamteua Chongolo kuwania ubunge.
Mkutano huo, uliwakutanisha jukwaa moja Dk Nchimbi na Chongolo ambao wamehudumu nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM kwa nyakati tofauti. Chongolo alimwachia kijiti Dk Nchimbi ambaye naye amemwachia Dk Asha-Rose Migiro.
Dk Nchimbi akijibu kero ya soko na stendi ameanza kwa kusema:”Namshukuru ndugu yangu, mgombea wetu wa ubunge, Daniel Chongolo. Tunamfahamu kama mchapa kazi na tutashirikiana naye vizuri.”
“Tunakwenda kujenga soko la kisasa, Mambakambo na Makambako inaunganisha nchi na mataifa mbalimbali, tunakwenda kujenga stendi ya kisasa,” amesema Dk Nchimbi.
Hoja ya mazingira bora ya wafanyabiashara, Dk Nchimbi amesema:”Makambako ni wafanyabiashara kama alivyosema mgombea wetu wa ubunge kwamna wanahitaji sera rafiki za TRA, sera rafiki za kodi, tunakwenda kusimamia sera ili walipe kodi na kodi stahiki na siyo kodi za kubambikiziana.”
Amesema wanakwenda kujenga vituo vingine vya afya viwili, zahanati tatu na kuboresha hospitali ya Wilaya. Madarasa 241 yatajengwa, miradi ya maji itatekelezwa:”Tunataka kumaliza kabisa tatizo la maji Makambako.”
“Mbunge wetu amesema vizuri habari ya barabara. Barabara alizozitaka mgombea wetu wa ubunge, tutashirikiana naye kutafuta majibu, lengo la mbunge wenu ni kuandika historia ya Njombe na jimbo lake la Makambako,” amesema huku akishangilia.
Dk Nchimbi amesema hayo yote na mengine mengi watayatekeleza iwapo tu wananchi watajitokeza kwa wingi Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kumchagua Samia kuwa Rais, mbunge wao Chongolo na madiwani.
Baada ya ahadi hizo, Mwananchi limezungumza na Julius Kibiki, Mkazi wa Mangole ambaye amesema:”Stendi ikijengwa na soko likijengwa italeta tija kubwa kwani kwa sasa soko lililopo limejengwa miaka ya nyuma limechakaa.”
“Mvua ikinyesha hakuna pa kusimama na ikijengwa watakuwa wametutatulia tatizo hili ambalo limekaa muda mrefu. Kikubwa watekeleze tu ahadi,” amesema Kibiki.
Naye David Mbwilo, Mkazi wa Makambako amesema iwapo stendi na soko vikijengwa, vitaongeza thamani ya mji huo na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
“Najua hilo soko litakuwa la kisasa, tutapata maduka ya kuuza vitu na hiyo stendi nayo inaweza kuwa ya kisasa, hapo hata Halmashauri itaongeza vyanzo vya mapato,” ameswma Mbwilo.
Kuhusu Jah People, Dk Nchimbi amesema utaratibu wa chama hicho,
unapochukua fomu kugombea:”Unajua kuna kupata na kukosa, usipoteuliwa unakubali matokeo, namshukuru sana mwenyekiti wetu wa mkoa kwa kufanya kwa matendo na maneno.”
“Mgombea wetu (Chongolo) baada ya kuchaguliwa alionesha unyenyekevu mkubwa kwa wenzake,” amesema.
Mgombea ubunge wa Makambako, Daniel Chongolo amesema jimbo hilo ni mji wa biashara na wananchi hawana muda wa kuomba omba, kila mmoja hapa mkutanoni ana shughuli yake ya kujiingizia kipato.
Chongolo amesema mwaka 2020 kulikuwa na barabara nyingi zenye vumbi lakini sasa zimepungua na kwa ushirikiano wake na madiwani watahakikisha wanasukuma kuzimalizia.
“Najua mlango wako (Dk Nchimbi) utakuwa wazi kuja kufikisha kero za wananchi, kwani najua mimi nilikuachia kijiti cha ukatibu mkuu, sidhani kama utakataa kunipokea,” amesema Chongolo.
Miongoni mwa barabara zinazohitaji kujengwa ni ya Iringa na Barabara inayoanzia Kwa Mgimba kwenda Hospitali ya Mlowa, bado kilomita chache:”Na niwahakikishe tutafika Hospitali kwa lami.”
Katibu mkuu huyo wa zamani wa CCM amesema kuna barabara inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya nyanda za juu, Njombe Mjini hadi Ruvuma na inakwenda hadi mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi, Zambia, Malawi na Congo.
“Barabara hii kwa sasa inapitisha malori mengi kwenda Songea. Tunaomba sana tuiboreshe ili iwe ya kisasa na itafungua mji wetu wa Makambako,” amesema Chongolo.
Aidha, amesea stendi mpya na ya kisasa ya Makambako na soko vikijengwa itasaidia kuupamba mji huo:”Kwani saizi mtu akija Makambako, ukimuuliza uko wapi, atasema kwenye stendi ya tenki, sasa soko na stendi mpya ikikamilika, tutaufanya mji uwe wa kisasa zaidi.”
Amesema tumekuwa hatuna chuo, lakini Serikali inayoongozwa na Rais Samia:”Tunashukuru kutuletea Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na sisi Makambako tumetoa eneo la ekari 100 bure, hii itaongeza mazungumzo wa fedha.”
“Nisiposema jambo kuhusu Mzee wangu Jah People nitakuwa nakosea, nilipokuwa nasema mafanikio ndiyo wao wameyasimamia haya na madiwani, sasa nimepokea kijiti kwa sababu mimi ni kijana niende kasi, tunamshukuru sana Mzee wangu Jah People,” amesema Chongolo huku akishangiliwa.

Awali, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Njombe, Deo Sanga maarufu Jah People amesema wakati Mjumbe wa Kamati Kuu, Salum Asas anasema kwamba nitapita kufanya kampeni kwa ajili ya mdogo wangu (Chongolo), niseme yule ni mtoto wangu, hata alipokuwa anakwenda kuchukua fomu ya ubunge nilikwenda naye na ile fomu nilimlipia mimi.
“Sasa yale mambo yamekwisha na sasa ni Daniel Jah People, kwa hiyo nimembatiza anaitwa Daniel Jah People Chongolo na nitapita kule kumwombea kura.
Na niliwaambia mambo yale yameisha na sasa amepewa nafasi hiyo na jimbo hili sasa litakimbia kasi kubwa na atakayekimbiza ni Daniel Jah People Chongolo,” amesema Jah People huku shangwe likiibuka mkutanoni hapo.
Katika mkutano huo, Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema kila baada ya miaka mitano, tunachagua viongozi:”Na wengi wenu hapa tunafahamiana, nilikuwa kule nikasepa na kuja CCM.”
“Kauli mbiu yetu mwaka huu ni kazi na utu, Mheshimiwa Samia anapoongeza vituo vya afya, anapoleta maji, anapoboresha huduma za afya hiyo ni kazi na utu, anapoongeza madarasa ili watoto wasome hiyo ni kazi na utu.”
Amesema Serikali ya CCM inapotatua changamoto za wananchi ikiwemo kusogeza huduma karibu na makazi ikiwemo kuboresha shughuli za usafirishaji:”Hiyo ndiyo kazi na utu. Yaani unafanya kazi huku ukizingatia utu wa wananchi na ndiyo Mheshimiwa Samia anachokitaka.”
Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa Mbunge wa Iringa Mjini na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema amesema:”Serikali ya CCM ina hakikisha wananchi wanyonge kama Mwalimu Nyerere alivyosema tunasaka uhuru ili kukomesha ujinga, umasikini na maradhi na sasa CCM chini ya Rais Samia anaendelea Kupiga kazi na utu unawekwa mbele.”
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kutoka Mkoa wa Ruvuma, Hemed Chale amesema kazi kubwa umefanyika katika kila eneo mathalani ya kumtua mama ndoo kichwan akisisitiza maeneo mbalimbali miradi inatekelezeka.

Amesema kazi iliyoanzishwa miaka minne na nusu iliyopita na Rais Samia:”Tukaiendeleze na ili iendelee Oktoba 29 tujitokeze kwa wingi kuchagua mafiga matatu, Rais, wabunge na madiwani wa CCM.”
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Leonard Qwihaya amesema Makambako ni mji wa kijaja na amewaomba kila mmoja uhakikisha wanawahamasisha kila mmoja aliyejiandikisha kwenda kupiga kura.
Qwihaya amesema si wote waliojiandikisha ni wana CCM:”Hivyo, tuwachukue na kwenda nao, kisha tuwaelimishe jinsi ya kukipigia kura chama chetu kwani si wote ni wana CCM, nawaomba sana tuhamasishane na tukitokeze kwa wingi.”
Mjumbe wa Kamati Kuu na Mratibu wa kampeni mikoa ya kanda ya nyanda za juu, Salum Asas amesema:”Hapa tuna makatibu wakuu wawili, mmoja ni mgombea mwenza na mwingine ni mgombea ubunge wa Makambako. Tuna bahati kuwa na makatibu wakuu wastaafu kwenye jukwaa moja, hii ni bahati sana.”
Asas amesema mbunge wa zamani wa Makambako ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga maarufu Jah People amesea Sanga atafanya kazi ya kutafuta kura ili kumwachia kijiti mdogo wake Chongolo na huu ndiyo utaratibu wa CCM.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua yanayotokea kwenye mikutano yake