Muheza. Wakati Mkoa wa Tanga hasa Wilaya ya Muheza ikisifika kwa uzalishaji wa machungwa, maembe na mananasi nchini, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimeahidi kuja na kiwanda cha kutengeneza juisi itokanayo na matunda hayo.
Kiwanda hicho kitakuza ajira kuanzia kwa wakazi wa eneo hilo, mnyororo mzima wa kiuchumi kukua pamoja na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla.
Hiyo ni miongoni mwa ahadi iliyotolewa na wagombea wa Chaumma leo Alhamisi Septemba 25, 2025 Kata ya Tanganyika jimbo la Muheza kwenye mkutano wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza mgombea mwenza wa urais wa Chaumma, Devotha Minja, amesema haiwezekani mkoa huo usifike kwa uzalishaji wa matunda ya nanasi, maembe na machungwa halafu juisi itoke nje ya nchi akitolea mfano Afrika Kusini.
“Muheza mmejaaliwa kuwa na matunda mengi, Chaumma tukiingia tu madarakani tunakuja na viwanda vya kuchakata juisi za matunda yanayopatikana hapa, wakulima wetu wanufaike,” amesema.
Faida mojawapo ya viwanda vya matunda hayo ni wakulima kuuza matunda hayo moja kwa moja viwandani wanufaike wakuze uzalishaji kisha watajirike.
Sambamba na hayo yote Devotha ameahidi kutengeneza mazingira bora ya kina mama kujifungua, miundombinu, maji pamoja na elimu.
Mgombea Ubunge wa jimbo hilo Yosepher Komba amesema ujio wa kiwanda hicho una tija kuliko inavyodhaniwa hivyo akiingia madarakani jambo la kwanza ni viwanda.
“Muheza inasifika kwa matunda tukija na kiwanda hapa watu watapata ajira. Haiwezekani wakulima wahangaike kulima halafu wasinufaike na zao hilo,” amesema.
Amesema kiwanda hicho mbali ya kukuza uchumi kitaongeza uzalishaji wa matunda hayo zaidi .
Kujengwa kwa viwanda vya matunda kumetajwa kutanufaisha mnyororo mzima wa kiuchumi kuanzia mama lishe, bodaboda, wachimbaji wenyewe wafanyakazi viwandani na Serikali kwa ujumla.
Akieleza kuhusu mikakati ya Chaumma Tanga, amesema watajenga miundombinu, ajira, bima ya afya kwa wote, pamoja na vituo vya afya katika kata zote.
Chaumma inaahidi hayo wakati kampeni za uraisi, wabunge na madiwani zinaendelea kuchanja mbuga kote nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
“Pia, ntahakikisha mikopo inawafikia walengwa, maji yanapatikana sio kama ilivyosasa, elimu pamoja na barabara zote za jimbo kuwa za viwango bora vya lami.