Diarra kweli nimeamini avumae baharini papa

SASA hivi Yanga wanatamba kumchapa mtani wao Simba katika mechi sita mfululizo za mashindano tofauti ambayo ni Ligi Kuu Tanzania Bara na Ngao ya Jamii.

Ni haki yao kutamba kiukweli maana hizi ndio timu mbili kubwa na utani wao wa jadi ni wa muda mrefu hivyo unavyompata mwenzako unapaswa utembee kifua mbele haswa maana siku ya wewe kupatikana utakiona cha moto.

Katika vipigo hivyo vyote mfululizo ambavyo Yanga imevitoa kwa Simba, kuna wachezaji tofauti ambao kijiwe kinaona wamekuwa wakipata sana ujiko upande wa Jangwani kwa maana ya kuona mchango wao mkubwa umesaidia kumpiga mtani.

Mwamba ambaye anatajwa sana ni Pacome Zouzoua ambaye tangu aje nadhani ameshaifunga Simba kama mara tatu hivi tofauti huku akipiga mpira mwingi na amekuwa akiwapa jeuri sana Yanga kila wanapoingia katika dabi.

Halafu kuna Maxi Nzengeli na siku hizi kaibuka Clement Mzize ambao kila mmoja amefunga bao katika hizo mechi ambazo Yanga imetoka kifalme dhidi ya Simba pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia msimu wa 2023/2024, 2024/2025 na huu ambao umeanza.

Hata hivyo, kuna mtu mmoja ambaye pengine inawezekana akawa ameziamua kwa kiasi kikubwa mechi hizo sita za Kariakoo Dabi ambaye ni kipa Djigui Diarra wa Yanga anayedakia pia timu ya taifa ya Mali.

Diarra katika hizo mechi sita amefanya sevu za maana ambazo baadhi kabla zilionekana kama zilikuwa nafasi kwa Simba kufunga mabao, lakini uhodari wa Diarra ukaiweka mchezoni Yanga na mwishoni ikaibuka na ushindi.

Mfano kuna ule mchezo ambao Diarra alimhadaa Leonel Ateba na kuokoa shambulizi lake wakati mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba alipotaka kujaribu kumpiga chenga ili apate fursa ya kuiandikia timu yake bao. Ateba angeweka kambani chuma ile pengine yangekuwa yanasemwa mengine.

Kumbuka mechi ya juzi ya Ngao ya Jamii zile nafasi nne za wazi ambazo Diarra aliokoa kutokana na mashambulizi ya Shomari Kapombe, Kibu Denis na Charles Ahoua. Jamaa kipa sana.