Elimu ya fedha kupitia maudhui yanayopendwa na wengi

Katika utoaji wa elimu, njia na mbinu za kufikisha ujumbe ni jambo la msingi. Zikitumika ipasavyo, husaidia maarifa kupokelewa kwa urahisi na kueleweka kwa kundi kubwa la watu kwa muda mfupi.

Vilevile, katika huduma za kifedha, utoaji wa elimu unapata msisitizo mkubwa kutokana na mabadiliko makubwa yanayoendelea katika sekta hii.

Ikiwa elimu ya fedha itafungamanishwa na maudhui yanayopendwa na Watanzania wengi, itaongeza kasi ya uelewa na kuwahamasisha zaidi kutumia huduma rasmi za kifedha. Hatua hii itasaidia ufikishaji elimu hiyo kufika kwa uharaka na kutoa tija nzuri.

Kwa kuzingatia muktadha wa jamii yetu, jambo hili ni muhimu kwa sababu kadhaa. Kwanza, matumizi ya huduma za kifedha bado ni dhana mpya.

Hadi leo, shughuli kama vile kuweka akiba, kukopa, kutuma na kupokea fedha, kwa wengine hufanyika kwa njia zisizo rasmi. Hii inaonyesha haja ya kuelimisha watu kwa namna ambayo hawataiona kama tangazo au kushawishiwa kibiashara.

Mfano mzuri ni kutumia michezo ya maigizo ya Kiswahili ambayo hupendwa na wengi kama njia ya kufikisha elimu ya fedha. Wakati mtazamaji akifuatilia tamthilia yake pendwa, ujumbe wa kifedha unaweza kuingizwa kwa uhalisia unaoendana na maisha ya kawaida.

Mathalan, inaweza kuonesha namna mtu anavyofanya kazi, anatunza fedha zake, anafungua kampuni, anasimamia biashara au kulipa kodi. Na si michezo ya maigizo yanayoonesha anasa na ufahari tu!

Bali inajikita katika uhalisia wa maisha na kuwasaidia watu kujifunza mbinu sahihi za kifedha kwa namna rahisi na kumfanya mfuatiliaji au mtazamaji apokee taarifa bila kujihisi kama ametangaziwa moja kwa moja na benki au taasisi ya kifedha.

Pili, kundi kubwa la watumiaji wa huduma za kifedha lipo mitaani, nje ya mfumo rasmi wa elimu. Kwa kawaida, elimu ya fedha hutolewa kupitia semina, midahalo, vipeperushi, majarida au matangazo.

Njia hizi hutegemea zaidi tabia ya watu kupenda kusoma na kufuatilia maandiko, lakini ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya wananchi haipo kwenye utamaduni huo. Utaskia, ondoa hilo tangazo, na mengine.

Iwapo elimu ya fedha itaingizwa kwenye maudhui yanayopendwa kwa mfano muziki, ambayo ni chombo chenye ushawishi mpana. Ujumbe wa kifedha ukichanganywa kwenye wimbo maarufu, au kuoneshwa kupitia mitindo ya maisha ya wasanii na watu maarufu, unaweza kufika mbali zaidi.

Hii inaweza kuleta mabadiliko ya kitabia na kuongeza uelewa wa kifedha haraka kwa mbalimbali ya kijamii, watoto. vijana, watu wazima, nk.

Tatu, utoaji wa huduma za kifedha mara nyingi hutumia misamiati ya kitaalamu, na mara nyingine lugha ya Kiingereza. Hali inayoweza kuwafanya watu wengi washindwe kuelewa kwa undani au kutotilia maanani ujumbe, na matokeo yake ni kukosa manufaa ya maarifa yaliyokusudiwa.

Lakini pale elimu ya fedha inapochanganywa na maudhui yanayopendwa. Fikiria mfano wa mpira wa miguu: wakati wa uchambuzi au ushabiki, elimu ya fedha inaweza kuingizwa kwa ustadi kama vile kuhamasisha bima, kufundisha namna rahisi ya kuweka akiba, au kueleza jinsi ya kulipa ada kwa simu.

Kauli nyepesi kama “jilinde kwa bima kimwananchi!” au “nunua jezi kwa simu” zina nguvu ya kuwafikia mashabiki.

Aidha, sekta ya michezo yenyewe inaweza kubeba elimu ya kifedha kwa kubuni vipindi au mijadala inayohusisha uchumi wa michezo: biashara ya klabu, ada za usajili, mikataba ya wachezaji, au mapato ya matangazo.

Hivyo, mazungumzo ya kishabiki hayatalenga tu nani kafunga goli, bali pia yataongeza uelewa wa masuala ya kifedha yanayoathiri maisha ya kila siku ya wachezaji na mashabiki.

Kwa kumalizia, taasisi za kifedha zina nafasi ya pekee ya kushirikiana na wabunifu wa programu, waandaaji wa matukio ya michezo na muziki, pamoja na wataalamu wa lugha ya Kiswahili ili kubuni mbinu mahususi za kuongeza wigo wa elimu ya fedha.

Kupitia ushirikiano huu, elimu inaweza kufikishwa kwa njia mbadala ndani ya maudhui yanayopendwa na wananchi wengi. Hatua hii si tu itarahisisha upokeaji wa maarifa, bali pia itahakikisha elimu ya fedha inakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya jamii.