Fedha za kampeni kutoka Libya zampeleka jela rais mstaafu Ufaransa

Paris. Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy (70), amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya ufadhili haramu wa kampeni za urais mwaka 2007, kwa kutumia fedha kutoka kwa serikali ya aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.

Hukumu hiyo ya hatia inamaanisha kuwa Sarkozy, aliyeongoza Ufaransa kati ya mwaka 2007 na 2012 na alistaafu siasa rasmi mwaka 2017, atalazimika kutumikia kifungo hicho hata kama atakata rufaa.

Sarkozy alishtakiwa kwa kufanya makubaliano na Gaddafi mwaka 2005, alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ili kupata ufadhili wa kampeni yake kwa kubadilishana na kumuunga mkono Gaddafi katika jukwaa la kimataifa, wakati Libya ilikuwa ikitengwa na mataifa mengine.

Rais huyo wa zamani amekana mashtaka yote na kudai kuwa kesi hiyo ina msukumo wa kisiasa.

Sarkozy tayari ametangaza kuwa atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, aliyoielezea kama nzito mno kwa utawala wa sheria.

Akizungumza baada ya kusikiliza hukumu hiyo leo  Alhamisi, Septemba 25, 2025, amedai kesi hiyo ina msukumo wa kisiasa, huku upande wa waendesha mashtaka ukidai Sarkozy aliahidi kumsaidia Gaddafi kurekebisha sifa yake mbaya mbele ya mataifa ya magharibi kama malipo ya msaada huo wa kifedha.

Katika unafuu mdogo kwake, Mahakama ya Jinai ya Paris iliagiza kuwa, Sarkozy asiwekwe rumande kwanza na waendesha mashtaka wamepewa muda wa mwezi mmoja kumjulisha lini ataanza kutumikia kifungo chake.

Jaji Nathalie Gavarino amesema kuwa Sarkozy amehukumiwa kwa sababu aliruhusu wasaidizi wake wa karibu kutafuta msaada wa kifedha kutoka utawala wa Libya.

Wasaidizi wawili wa karibu wa Sarkozy alipokuwa rais, mawaziri wa zamani Claude Guéant na Brice Hortefeux pia walipatikana na hatia ya kushiriki katika njama ya jinai, lakini wakasamehewa katika mashtaka mengine.

Eric Woerth, aliyekuwa mweka hazina wa kampeni ya Sarkozy mwaka 2007, aliachiliwa huru.

Jaji Nathalie Gavarino alisema Sarkozy, akiwa waziri na kiongozi wa chama wakati huo, aliwaruhusu washirika wake wa karibu na wafuasi wa kisiasa aliokuwa na mamlaka nao kuwasiliana na maofisa wa Libya kwa niaba yake ili kupata au kujaribu kupata msaada wa kifedha.

Hata hivyo, Mahakama haikukubaliana na hitimisho la waendesha mashtaka kwamba Sarkozy alinufaika moja kwa moja na ufadhili huo haramu wa kampeni.

Kesi hiyo ilianza mwaka 2011, baada ya Shirika la Habari la Libya na Gaddafi mwenyewe kudai kuwa serikali ya Libya ilitoa mamilioni ya euro kwa siri kufadhili kampeni ya Sarkozy mwaka 2007.

Mwaka 2012, jarida la uchunguzi la Ufaransa Mediapart lilichapisha kile lilichodai kuwa, ni kumbukumbu ya kijasusi ya Libya ikielezea makubaliano ya ufadhili wa Euro 50 milioni.

 Sarkozy alikanusha nyaraka hiyo na kuwashtaki kwa kashfa.

Ushahidi mwingine uliowasilishwa katika kesi hiyo ni pamoja na taarifa kutoka kwa maofisa saba wa zamani wa Libya, safari za Gueant na Hortefeux kwenda Libya, miamala ya kifedha na madaftari ya waziri wa zamani wa mafuta wa Libya, Shukri Ghanem, aliyekutwa amekufa maji katika Mto Danube huko Vienna mwaka 2012.

Waendesha mashtaka walidai kuwa, Sarkozy alinufaika kwa makusudi kutokana na kile walichokiita mkataba wa rushwa, kati yake na serikali ya Gaddafi.

Kiongozi huyo wa muda mrefu wa Libya aliangushwa na kuuawa na wapinzani wake mwaka 2011 wakati wa vuguvugu la Arab Spring, huku Ufaransa chini ya Sarkozy ikishiriki kwa kiwango kikubwa katika operesheni ya Nato ya kutekeleza eneo la marufuku ya ndege.

Msururu wa matatizo ya kisheria

Sarkozy amekumbwa na matatizo mengi ya kisheria tangu amalize kipindi chake cha urais.

Amewahi kufunguliwa mashtaka tofauti ya rushwa, kutumia ushawishi vibaya na ukiukaji wa sheria za ufadhili wa kampeni.

Alihukumiwa kwa mara ya kwanza kwa kosa la rushwa na kupewa kifungo cha mwaka mmoja, alichokitumikia nyumbani kwa kuvaa kifaa cha kielektroniki (electronic tag) kwa miezi mitatu kabla ya kupewa msamaha wa masharti.

Katika kesi tofauti ya ‘Bygmalion’ alipatikana na hatia ya kutumia zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa cha fedha katika kampeni yake ya uchaguzi ya mwaka 2012 na kuficha matumizi hayo na alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja.

Pia, amekumbana na athari nje ya Mahakama, ikiwa ni pamoja na kupoteza Tuzo ya Heshima ya Taifa ya Ufaransa (Legion of Honour) baada ya hukumu ya rushwa.

Hata hivyo, rais huyo wa zamani bado ana ushawishi mkubwa na umaarufu katika siasa za mrengo wa kulia Ufaransa na anafahamika kuwa hukutana mara kwa mara na Rais Emmanuel Macron.

Sarkozy na mkewe Carla Bruni

Sarkozy aliwasili mahakamani akiwa ameongozana na mkewe, mwanamuziki na mwanamitindo Carla Bruni-Sarkozy na kuingia katika ukumbi wa Mahakama uliojaa waandishi wa habari na umma.

Aliketi mstari wa mbele wa viti vya washtakiwa. Wanawe watatu wakubwa pia walikuwepo ukumbini.

Licha ya kashfa mbalimbali za kisheria zilizogubika urithi wake wa kisiasa, Sarkozy bado ni mtu mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za mrengo wa kulia nchini Ufaransa na pia katika duru za burudani kupitia ndoa yake na Bruni.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao