KIUNGO mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’, amehitimisha rasmi siku 297 za ukame wa mabao ya Ligi Kuu, baada ya nyota huyo kufunga bao moja katika ushindi wa kikosi hicho wa 2-0, dhidi ya Mbeya City kwenye Uwaja wa Azam Complex.
Katika mechi hiyo, Feisal alifunga bao ambalo ni la pili kwa Azam dakika ya 46, akipokea pasi ya Baraket Hmidi, baada ya Nassor Saadun kukitanguliza kikosi hicho dakika ya 32, akipokea mpira uliopigwa na kiungo nyota, Abdul Suleiman ‘Sopu’.
Kabla ya bao hilo, mara ya mwisho kwa nyota huyo kufunga ilikuwa ni katika ushindi wa Azam wa mabao 3-1, dhidi ya Dodoma Jiji ugenini, mechi iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Desemba 1, 2024, hivyo kuhitimisha rasmi siku 297.

Fei Toto ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024 na alichangia mabao 27 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimzidi, Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga, aliyefunga 12 na kuasisti tisa.
Mwaka 2024, Feisal aliongoza kwa nyota waliochangia mabao mengi, akifuatiwa na Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga ambaye kwa sasa yupo Wydad Casablanca ya Morocco na hadi anaondoka alichangia 21, baada ya kufunga 12 na kuasisti tisa.

Kiwango bora cha Feisal kilimfanya kumaliza na mabao 19 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023-2024, akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kufunga mabao mengi zaidi, nyuma ya Aziz KI wa Yanga aliyefunga jumla ya mabao 21.
Pia, alikuwa mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho (FA), msimu wa 2023-2024, kwa kuifikisha Azam fainali na kuchapwa na Yanga kwa penalti 6-5 baada ya suluhu ya (0-0) ya dakika 120 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar Juni 2, 2024.

Mbali na hilo pia, Feisal aliiwezesha Azam kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 10, tangu mara ya mwisho kikosi hicho kiliposhiriki mwaka 2015, kufuatia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014.
Timu hiyo ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024-2025, baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara na pointi 63, ingawa kikosi hicho kiliishia hatua ya awali, baada ya kuondolewa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1.
Msimu uliopita wa 2024-2025, Feisal akiwa na kikosi hicho cha Azam, alichangia mabao 17 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga mabao manne na kuasisti mengine 13, akiwa ni asisti nyingi kuliko yeyote.

Akizungumza baada ya mechi na Mbeya City, Kocha wa Azam, Florent Ibenge, alisema amefurahishwa na mwendelezo mzuri wa nyota wa kikosi hicho, kutokana na jinsi wote wanavyofuata maelekezo yake vizuri na kuyafanyia kazi uwanjani.