GCAP YAISHAURI SERIKALI KUCHUKUA HATUA MADHUBUTI KUTEKELEZA SDGS

 ::::::::::

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Mtandao wa GCAP Tanzania umetoa wito kwa Serikali, asasi za kiraia,
sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti na jumuishi
kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa vitendo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mjumbe wa GCAP
kutoka shirika la Dayspring Foundation, Rosemary Mwaipopo, alisema ni lazima
haki za binadamu zilindwe na maendeleo yawe shirikishi kwa makundi yote,
ikiwemo wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

Alizitaka asasi za kiraia kupaza sauti za wananchi, sekta binafsi
kuwekeza kwenye ajira zenye staha, na Umoja wa Mataifa kusaidia zaidi kupitia
rasilimali na ushirikiano wa kiufundi. Aidha, aliihimiza Serikali kuhakikisha
sera na bajeti zake zinajielekeza kwenye uchumi jumuishi.

Kwa upande wake, Martina M. Kabisama kutoka GCAP Tanzania Coalition,
alisema licha ya hatua zilizopigwa, changamoto kama umasikini, ukosefu wa
usawa, na athari za mabadiliko ya tabianchi bado ni kubwa.

Alisema vijana zaidi ya 800,000 huingia sokoni kila mwaka lakini wengi
huishia kwenye ajira zisizo rasmi, huku hifadhi ya jamii ikiwafikia Watanzania
wachache.

GCAP imesisitiza haja ya kuweka kipaumbele katika uongozi bora,
ushirikishwaji wa wananchi, na kupunguza pengo la kiuchumi ili kufikia dira ya
maendeleo ya 2050 na kutimiza SDGs ifikapo mwaka 2030.