Jenerali Mkunda Ampongeza Sajinitaji Simbu  – Global Publishers



Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda amempongeza Sajini Alphonce Simbu kwa ushindi wa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Mbio za  Marathon ya Dunia kilomita 42 zilizofanyika Jijini Tokyo Japan.

Pamoja na pongezi hizo,

Jenerali Mkunda amempandisha cheo kutoka Sajini kuwa Sajinitaji tukio lililofanyika ofisini kwake  Makao Makuu ya Jeshi Upanga Jijini Dar es Salaam tarehe 25 Septemba 2025.

Amesema ushindi huu ni kwa watanzania wote na Afrika kwa ujumla na kwamba  michezo ni sehemu ya kazi jeshini hivyo Sajinitaji Alphonce Simbu amefanya kazi nzuri.

Jenerali Mkunda ametoa rai kwa Maafisa na Askari wote jeshini waige mfano wa Sajinitaji Simbu kwa kufanya kazi kwa bidii na kuleta mafanikio katika kila idara jeshini.

Naye, Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema safari hii katika michezo  Jeshi limefanya vizuri sana ambapo tarehe 26 Septemba 2025 Katika Uwanja wa Golf Lugalo,  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi atapokea vikombe kutoka timu za Jeshi zilizofanya vizuri katika Mashindano

mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA), Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF CUP) na Medali aliyoipata Sajinitaji Alphonce Simbu.