JUMA ALI KHATIBU: Mgombea anayepiga hesabu za Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar

Nyakati za uchaguzi, wagombea hujitokeza kila mmoja akiwa na dhamira ya aina yake. Zanzibar, mgombea urais kwa tiketi ya Ada Tadea, Juma Ali Khatib, anasema kuwa Wazanzibari wanapaswa wamwelewe kwamba amejitosa kuwania urais ili aibuke nafasi ya pili na apate asilimia zitakazomwezesha kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia marekebisho ya mwaka 2010, ibara ya 39 (3), kifungu kidogo (I), inaeleza kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, atateuliwa iwapo chama chake kitapata asilimia 10 au zaidi ya kura za urais. Juma ameingia ulingoni kuwania urais, aweze kupata kura hizo, ili zimpe sifa ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Anasema mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Ali Mwinyi ambaye ndiye Rais wa Zanzibar, akiwania muhula wa pili, amefanya vema kwenye uongozi wake muhula wa kwanza. Anataja miundombinu kama eneo ambalo Rais Mwinyi amelifanikisha kwa ubora wa hali ya juu. Juma anachoomba, Mwinyi aendelee kuwa Rais yeye awe makamu wa kwanza wa Rais akamsaidie kazi.

Huyo ni Juma, kama wazazi wake wangeamua, basi wangemwita Mapinduzi. Ni kwa sababu alizaliwa siku ya kilele cha Mapinduzi Zanzibar, Januari 12, 1964. 

Hata hivyo, mzee Ali Khatib Khamis na mkewe, Mariam Mohamed Haji, waliamua kumwita Juma.

Asili ya Juma ni Wilaya ya Mkoani, Pemba, Zanzibar. Wazazi wake walikuwa wakiishi Pemba, lakini kipindi mama yake alipokuwa na ujauzito, alifanya safari ya kutembelea Unguja. Na akiwa Unguja, aliishi eneo la Kisima Majongoo, Mjini Magharibi, Unguja.

Mariam alipotaka kurejea Pemba baada ya kumaliza siku za matembezi, mume wake (Ali), alimwambia asubiri ajifungue. Na hiyo ikawa sababu ya Juma kuzaliwa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Wilaya ya Mjini, Unguja.

Simulizi ya Juma siku alipozaliwa ni kuwa alizaliwa alfajiri ya Januari 12, 1964. Muda mfupi baada ya mama yake kujifungua, makumi ya watu walipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja wakiwa wamejeruhiwa. Wapo waliokuwa wamekatwa miguu, wengine mikono, damu zikiwavuja, na wachache walikuwa wameshafariki dunia.

Baada ya kuona hali hiyo, huku Hospitali ya Mnazi Mmoja ikiwa imezidiwa na majeruhi wa matukio ya Mapinduzi, Mariam (mama Juma), alipelekwa na mwanaye kwa gari la jeshi hadi Kisima Majongoo, alikokuwa amefikia. Hivyo ndivyo Juma alivyozaliwa na kupata nusura ya uhai wake.

Mariam alirejea Pemba na mwanaye, Juma. Mzee Ali aliwapokea Pemba. Maisha yakaendelea kutoka hapo.

Mwaka 1970, Juma alianza darasa la kwanza, Shule ya Msingi ya Uweleni, iliyopo Wilaya Mkoani, Kusini Pemba. Alihitimu darasa la saba mwaka 1976.

Kutoka Uweleni alikohitimu elimu ya msingi, mwaka 1977, Juma alijiunga na Shule ya Sekondari ya Fidel Castro.

Mwaka 1980, Juma alihitimu elimu yake ya sekondari na baada ya hapo, hakuendelea na masomo, badala yake alianza kujifunza kazi ya ushonaji kwa kutumia cherehani na kugeuka fundi hodari ya cherehani.

Kati ya mwaka 1981 mpaka 1982, ungemkuta Juma akiwa fundi mahiri wa kushona nguo za kiume na kike kwa kutumia cherehani, eneo la Kiponda, Mji Mkongwe, Unguja. Enzi hizo, hasa wakazi wa Kiponda, Mji Mkongwe, walimtambua zaidi kwa jina la ‘Fundi Juma.’

Mwaka 1982, Juma aliajiriwa Wizara ya Viwanda na Biashara Zanzibar, kama mshonaji wa viwanda vidogo. Juma alifanya kazi kwenye kiwanda cha ushonaji cha Amani, Zanzibar. Mwaka 1990, Juma aliacha kazi na kuanza kufanya biashara zake binafsi.

Mwaka 1993, Juma akiwa anajishughulisha zaidi na biashara zake, aliitikia wito wa kikisiasa. Alikuwa mmoja wanachama wa mwanzo wa chama cha Tadea (Tanzania Democratic Alliance), walioshiriki mapokezi ya mwanasiasa mkongwe nchini, Oscar Kambona, siku aliporejea nchini akitokea Uingereza alikokuwa akiishi ukimbizini.

Kambona baada ya kuwasili nchini na kukamilisha usajili wa kudumu wa Tadea, Juma alikuwa mmoja wa Wazanzibari wa mwanzo waliokibeba chama hicho kwa ajili ya kutafuta usajili wa kudumu.

Hivyo, popote unapomuona Juma, ujue unamzungumzia mwasisi wa Tadea na mmoja watu wa mwanzo kupokea siasa za mageuzi nchini katika mstari wa mbele.

Mwaka huohuo 1993, Juma aliteuliwa kuwa Naibu Katibu wa Uchumi na Miradi wa Tadea. Baadaye alichaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Tadea kwa Zanzibar, kisha akawa Katibu Mwenezi wa Tadea taifa.

Juma pia alishawahi kuwa Katibu Mkuu wa Tadea, wakati chama hicho kilipokuwa kinaongozwa na marehemu John Lifa Chipaka.

Juma alishapata kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tadea taifa. Na tangu mwaka 2017, alipofariki dunia Chipaka, Juma alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho. Uchaguzi Mkuu wa Ada Tadea uliofanyika Julai 2021, ulimchagua Juma kuwa Mwenyekiti wa chama hicho. Hivyo basi, Juma siyo tu mkuu wa chama, bali pia ndiye mkuu wa chama.

Linaweza kuwepo swali; ni kwa nini Tadea ilibadilika hadi kuitwa Ada Tadea? Jawabu ni John Shibuda. Mwaka 2015, mbunge huyo wa zamani wa Maswa Magharibi, alijiunga na Tadea.

Na pamoja na mambo aliyotaka kwa ajili ya mabadiliko ya chama, ni kutaka Tadea isiwe muungano wa kidemokrasia Tanzania, bali iwe Afrika nzima.

Ndipo neno ADA (African Democratic Alliance) liliongezwa, hivyo chama kikaanza kuitwa Ada Tadea na kutambulika hivyo hata kwa msajili wa vyama vya siasa. Ada Tadea, maana yake ni Ushirika wa Kidemokrasia Afrika na Ushirika wa Kidemokrasia Tanzania.

Mwaka 2015, Juma aligombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Ada Tadea. Hata matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015, yalipofutwa na kurudiwa Machi 20, 2016, Juma alikuwa mmoja wa wagombea wa vyama vya upinzani waliounga mkono marudio.

Mwaka 2016, Juma aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kisha Waziri Asiye na Wizara Maalum. Hivyo Juma ni mzoefu wa siasa za Zanzibar, maana ameshutoa huduma yake ndani ya Baraza la Wawakilishi, kadhalika Baraza la Mapinduzi.

Uchaguzi Mkuu 2020, Juma aligombea pia urais kwa tiketi ya Ada Tadea. Wakati huo, Rais aliyekuwa madarakani Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, alikuwa muhula wa mwisho ofisini. Hivyo Shein hakuwa anawania kiti cha Rais. Wakati huo, Juma aliwaomba Wazanzibari wamchague ili aendeleze miradi mingi ambayo iliachwa njiani na Shein.

Miaka mitano imepita, Juma anakuja wito mwingine. Hataki mashindano na Rais aliye madarakani. Anampongeza kwa kufanikisha maendeleo makubwa.

Juma anasifia uzuri na ubora wa barabara ambazo zimejengwa na Dk Mwinyi. Anamimina sifa kwa madaraja ya juu (flyovers), ambayo yamefanikishwa na Dk Mwinyi.

Juma anasema, Dk Mwinyi anahitaji wasaidizi bora, kwa hiyo anaomba wampigie kura nyingi apate asilimia za kumtosha kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, pia wawachague wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Ada Tadea, nao wakawe msaada kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Dk Mwinyi.