Kipigo chaizindua Pamba Jiji | Mwanaspoti

PAMBA Jiji jana usiku iliendeleza uteja wake mbele ya Yanga kwa kutandikwa mabao 3-0 na kuifanya timu hiyo katika mechi tatu za Ligi Kuu dhidi ya wapinzani wao kufungwa jumla ya mabao 10, kitu kilichomuamsha kocha wa timu hiyo kwa ajili ya mechi zijazo za ligi hiyo.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Muungano ilikumbana na kipigo hicho kwanza msimu huu kwenye Uwanja w Benjamin Mkapa na kocha Francis Baraza amekiri walizidi padogo na wanatumia matokeo hayo kama chachu ya kujipanga kwa mechi zijazo kabla ligi haijasimami kwa wiki mbili.

Awali Pamba ilianza kwa kutoka sare ya 1-1 na Namungo wiki iliyopita na kocha Baraza alisema kuvuna alama moja kupitia mechi mbili imemfanya kuwatia hasira wachezaji ili kupambana kwa mechi hiyo ikiwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza dhidi ya TRA United (zamani Tabora United).

Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema katika mechi ya juzi dhidi ya Yanga waliwazuia watetezi hao kwa mbinu walizozipanga kwa kuizuia eneo la kiungo, lakini ukomavu wa timu pinzani ndio umeamua matokeo mazuri.

“Ulikuwa mchezo mzuri na mgumu, nawapongeza wachezaji waliweza kufuata maelekezo yangu, ila  ukomavu wa Yanga ndio umetuhukumu na kujikuta tunapoteza kwa idadi kubwa ya mabao,” alisema kocha huyo raia wa Kenya na kuongeza;

“Mpango ulikuwa kuidhibiti Yanga eneo la kiungo kwa kiasi kikubwa tulifanikiwa, lakini wenzetu walitumia mbinu mbadala na kufanikiwa kupata matokeo kuna kitu nimejifunza kupitia mchezo huo.”

Baraza alitumia nafasi hiyo kumpongeza kocha wa Yanga, Romain Folz kwa kuisoma Pamba Jiji kikosi cha kwanza na kufanya mabadiliko ambayo yalikuwa na tija upande wao wakipata matokeo.

Baraza alisema wamesahau matokeo hayo sasa wanawekeza nguvu ya kurudi kujipanga mchezo unaofuata ambao wataikaribisha Tabora United mchezo na ameuitaja ndiyo utakaotoa picha ya ubora wa kikosi chake ambacho amesema kimekuwa kikicheza vizuri.

“Tunarudi nyumbani baada ya mechi mbili ugenini tukiambulia pointi moja, tuna mchezo ambao utapigwa mchana huu tutatumia kila njia kuhakikisha tunairudisha timu mchezoni kwa kuibuka na ushindi japo hatutarajii urahisi kutokana na ushindani uliopo.”

Kabla ya kipigo cha juzi Pamba iliyorejea Ligi Kuu msimu uliopita baada ya kuisoteza kwa mika 24 tangu iliposhuka mwaka 2001, ilipoteza pia nje ndani kwa watetezi hao ikianza kwa kichapo cha 4-0 Kwa Mkapa kabla ya kulala tena nyumbani kwa mabao 3-0.