Malindi ipo tayari kuivaa Chipukizi ZPL

KIKOSI cha timu ya Malindi, leo kinatarajia kusafiri kutoka Unguja kuelekea Pemba kwa ajili ya kucheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) dhidi ya Chipukizi itakayofanyika Septemba 27, 2025, kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani humo, saa 10:15 jioni.

Msafara wa timu hiyo utakuwa na watu 32 wakiwemo wachezaji 22, viongozi saba na waandishi wa habari watatu.

Wakati Malindi ikielekea Pemba, Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026 inaanza leo Septemba 25, 2025 kwa kupigwa mechi moja kati ya Polisi dhidi ya Uhamiaji kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja, saa 10:15 jioni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Malindi, Namala Suleiman amesema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na hakuna mwenye majeraha, hivyo kikosi hicho kipo tayari kukabiliana na mpinzani wake.

Namala amesema, anaamini mechi hiyo haitakuwa rahisi kwao kutokana na ukongwe na uzoefu wa Chipukizi ndani ya Ligi Kuu Zanzibar, hivyo wanatarajia kukutana na upinzani mkubwa.

Amefafanua kwamba, kati ya wachezaji wapya 21 waliosajiliwa msimu huu na timu hiyo, tisa wanatarajiwa kuonekana kwenye mechi hiyo.

“Tunachokitaka ni kuhakikisha tunacheza kwa umakini ili kushinda mechi hii ili tuondoke ugenini tukiwa na alama,” amesema.